September 24, 2025
Na Tullo Chambo, Riadha Tanzania.
MWANARIADHA wa Kimataifa wa Tanzania, Bingwa wa Dunia Marathon, Sajenti Alphonce Simbu, amekuwa kivutio kikubwa kwa wananchi mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam, mara aliporejea nchini akitokea Tokyo Japan.
Simbu, Septemba 16 mwaka huu, aliandika historia baada ya kuibuka Bingwa wa Dunia Marathon akitumia saa 2:09:48.03 katika Mashindano ya Dunia 'World Athletics Championship 2025 Tokyo Japan na kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano hayo makubwa kabisa duniani.
Simbu akiambatana na Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Rogath John na Kocha Denis Malle, alirejea nchini alfajiri ya Septemba 23 na kupata mapokezi makubwa yaliyoongozwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha sambamba na Naibu Mkurugenzi wa Michezo Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Kanali Penina Igwe.
Mara baada kuwasili, Simbu alipata mapumziko katika hoteli ya Blue Saphire Vingunguti na majira ya saa 4 asubuhi akiwa katika gari maalumu na msafara wa magari kadhaa ukiongozwa na Polisi wa Jeshi (MP), ulizunguka katika mitaa mbalimbali ya Dar es Salaam na kupita maeneo ya Karume, Kariakoo (Mzunguko wa Msimbazi), Mnazi Mmoja, Posta Mpya, Bandarini hadi hoteli ya Tiffany Diamond.
Simbu akiwa na medali yake ya dhahabu, akiwa juu ya gari akiwapungia wananchi waliokuwa pembezoni mwa barabara ambao walikuwa wamejaa shangwehuku wengine wakipigana vikumbo kumshika mkono na wengine kupiga naye picha huku wakimpongeza.
Kufika barabara ya Morogoro msafara wa Simbu ulipita mbele ya Shule ya Msingi Mtendeni ambapo wanafunzi walishindwa kujizuia na kupanda ukuta ili kumshuhudia.
Kivutio kingine alikuwa mwananchi mmoja mlemavu wa miguu, ambaye alikuwa amepandwa na hisia kali akitamani naye kumshika mkono Simbu, lakini akawa anashindwa kumfikia juu ya gari, kabla msamaria mmoja kumnyanyua na hatimaye kufanikisha azma yake ya kusalimiana na Bingwa huyo wa Dunia kwa staili ya kugonga naye 'tano'.
Msafara huo wa Simbu, pia ulipambwa na burudani ya matarumbeta kutoka kikundi cha Jeshi, ambacho kilikuwa burudani ya aina yake.
Hafla maalumu ya Simbu, inatarajiwa kufanyika Septemba 27 mwaka huu.