Health Nusu Marathon Kufanyika Dar Aprili 26

April 21, 2017


Katibu Mkuu wa Taasisi ya Tanzania Health Summit Bi. Rebecca John (katikati) akisisitiza jambo kwa wandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea maandalizi ya mbio za heart marathon na upimaji wa afya yenye lengo la kuisaidia serikali kupunguza magonjwa yasiyoambukizika mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Chama cha Riadha Tanzania Bi. Ombeni Zavara na kulia ni Katibu Mkuu Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Lucas Nkungu.
Katibu Mkuu Msaidizi wa Chama cha Riadha Tanzania Bi. Ombeni Zavara akizungumza na wandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya ya mbio za heart marathon na upimaji wa afya yenye lengo la kuisaidia serikali kupunguza magonjwa yasiyoambukizika mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Katibu Mkuu wa Taasisi ya Tanzania Health Summit Bi. Rebecca John.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Health Summit Dkt. Omary Chillo (kulia) akifafanua jambo kwa wandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea maandalizi ya mbio za heart marathon na upimaji wa afya yenye lengo la kuisaidia serikali kupunguza magonjwa yasiyoambukizika mapema hii leo jijini Dar es Salaam, katikati ni Katibu Mkuu Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Lucas Nkungu na kushoto ni Katibu Mkuu wa Taasisi ya Tanzania Health Summit Bi. Rebecca John.

……………..

Na Nuru Juma-Maelezo

Taasisi ya Tanzania Health Summit yaandaa mbio za nusu Marathon na Upimaji wa afya kwa lengo la kusaidia juhudi za serikali katika kupunguza magonjwa yasioambukiza, mbio hizo zinazotarajia kufanyika Aprili 26 katika barabara ya Kaole iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo Rebecca John wakati alipokutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuhamasisha jamii kushiriki.

“Kamati ya maandalizi ya ya mbio za Heart Marathon inapenda kuwa taarifu wadau wote wa sekta ya afya hapa nchini na jamii kwa ujumla juu ya mbio za Heart Marathon na upimaji wa afya ili kuungana na serikali katika juhudi za kupunguza magonjwa yasiyoambukiza” alisema Rebecca.

Aliongeza kuwa kwa mwaka huu mbio hizi zitashirikisha washiriki zaidi ya elfu mbili kutoka rika mbalimbali wakiwemo vijana, watoto, wazee, makundi ya watu wenye ulemavu na watu wenye magonjwa yasiyoambukiza.

Pia washiriki watapata nafasi ya kupima afya magonjwa mbalimbali kama vile shinikizo la damu ,wingi wa sukari katika damu, kiasi cha mafuta mwilini, uchunguzi wa uvimbe katika matiti na kupata ushauri wa wataalam kuhusiana na vyakula bora, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Aidha Bi. Rebecca aliongeza kuwa washiriki watakimbia umbali tofauti, kwani kuna mbio ndefu za kilometa 21.1 kwa ajili ya wakimbiaji wazoefu, kilometa 10 kwa wakimbiaji wa kati, kilometa 5 kwa wakimbiaji wa kawaida, kifamilia na kampuni na mbio za watoto chini ya miaka 12 ni meta 700 na zawadi itatolewa kwa mshindi wa kilometa 21.1 pekee kwa kiasi cha shilingi laki tano.

Kwa upande wake Rais wa Tanzania Health Summit Dr.Omary Chillo alisema kuwa washiriki watatakiwa kutoa kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kununua flana pamoja na kifaaa maalum cha kuhesabia muda wakati wa kukimbia ila maji ya kutosha yatatolewa bure kwa ajili ya wakimbiaji.

Aliongeza kuwa wameimarisha ulinzi kwa kushirikiana na jeshi la polisi na ili kulinda usalama kwa washiriki na wananchi watakaokuwepo katika mashindano hayo.

“wananchi wasiwe na wasiwasi wa usalama kwani tutashirikiana na jeshi la polisi ili kuimarisha usalama na tumeweza kupata baraka nyingi kutoka kwao kwa kuweza kushirikiana nao” aliongeza Chillo.

Pia Katibu msaidizi wa Chama cha Riadha nchini Bi Ombeni Zavala alisema anashukuru wananchi wanavyoweza kujitokeza katika mashindano hayo na pia anawaomba wananchi hasa vijana waendelee kujitokeza kwa wingi kwani wanaweza kupata nafasi ya kuunda timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17.

Naye Sajenti Isaya Mlokozi kutoka kanda ya usalama barabarani alisema jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani litahusika vizuri katika sehem inayowahusu kuhakikisha watu wanafanya zoezi hilo kwa hali ya usalama na litajumuika na wananchi popote pale watakapokuwa wanakwenda.

Mashindano haya mwaka jana yalifanyika katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam lakini kutokana na kuongezeka kwa watu mwaka huu yatafanyikia barabara ya kaole yenye kauli mbiu ‘piga hatua moja mbele ya magonjwa sugu’

RT Yataja Majina 23 Waliochaguliwa kuunda timu ya Taifa ya Vijana

April 17, 2017
Na Mwandishi Wetu
RIADHA Tanzania (RT) imetangaza majina 23 kwa ajili ya kuunda timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 kwa ajili ya kushiriki katika mashindano ya Kanda ya Tano ya Afrika yatakayofanyika jijini Dar es Salaam mapema mwezi ujao.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa RT, Whilhem Gidabuday, timu hiyo itapiga kambi katika hosteli za Filbert Bayi zilizoko Mkuza Kibaha kuanzia Jumanne chini ya makocha Robert Kalyahe na Mwinga Mwanjala.
Timu hiyo inaundwa na wachezaji 12 wavulana wakatu wasichana katika timu hiyo wako 11 ma watashiriki katika michezo yam bio za meta 100, 200, 400, 800, 1500 na 3000 pamoja na miruko na mitupo.


Gidabuday alisema kuwa kambi hiyo itagharimu kiasi cha sh Milioni 20 kuanzia timu hiyo itakapokuwa kambini kwa karibu siku 20, wakati wa mashindano na huduma zingine.


Mbali na wenyeji Tanzania Bara, nchini zingine zitakazoshiriki ni pamoja na Zanzibar, Uganda, Kenya, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia, Eritrea na Djibout.


Timu hiyo ilichaguliwa jana mara baada ya kumalizika kwa mashindano ya wazi ya taifa yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa na kuhudhuriwa na mikoa michache.
Baadhi ya wanariadha walioshiriki walitoka katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Arusha na Manyara, ambapo shule ya Filbert Bayi iliyopo mkoani Pwani, imeto wachezaji watano katika timu ya wasichana kutokana na umahiri wao.

Ukiondoa baadhi ya kasoro zilizokuwepo ikiwemo kutokuwa na huduma ya kwanza wala gari la wagonjwa, wachezaji wakishiriki bila ya kuwa na namba za kuwatambua na kuleta ugumu kwa waandishi wa habari kujua nani ni nani, mashindano yalienda vizuri.






















Mwanariadha wa Kimataifa, Alphonce Simbu Kuanza Safari ya Kushiriki London Marathon

April 17, 2017



Na Mwandishi Wetu

MWANARIADHA wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu kesho Jumatatu atapanda pipa kwenda Afrika Kusini akiwa njiani kwenda Uingereza, ambako atashiriki London Marathon Jumapili ijayo Aprili 23.

Simbu anapitia Afrika Kusini kwa ajili ya kupatiwa viza ya dharura ya kuingia Uingereza baada ya kuikosa ile ya kawaida jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday alisema jana kuwa, Simbu ataondoka kesho Jumatatu kwenda Afrika kusini kushughulikia viza ya kuingia Uingereza kabla ya kwenda nchini humo ambako Jumapili atashiriki London Marathon.

Simbu alifuzu kwa mbio hizo baada ya kumaliza katika nafasi ya tano katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Rio de Janeiro, Brazil 2016 kabla ya kushinda mbio za Mumbai Marathon.

Kwa mujibu wa Gida, tayari mwanariadha huyo ameingia katika orodha ya wanariadha bora kabisa duniani na ndio maana waandaaji wa London Marathon kuna fedha atapewa mara tu atakapoanza mbio hizo (Appearance Fees).

Gidabuday alisema kuwa Simbu hata kama hatashinda mbio hizo lakini akimaliza tu amejihakikishia fungu nono na kama akimaliza, basi ataondoka na maelfu ya dola za Marekani.

Simbu endapo atashinda mbio hizo za London Marathon ataondoka na kitita cha dola za Marekani 55,000 kama zaidi yash Milioni 150, na kama atafanikiwa kuvunja rekodi ataongezewa dola za Marekani 25,000 (ikiwa ni zaidi ya sh Mil 50),

Mshindi wa kwanza hadi wa 12 wa mbio hizo ataondoka na kitita cha fedha, huku wale watakaokimbia muda bora bbila kujali kama umevunja rekodi ya njia au ya dunia, nao wataongezewa fedha za bonasi.
 

Copyright © 2015 - 2025 Athletics Tanzania All Right Reserved

Developed by Gadiola Emanuel
Theme By AP | Developed By Gadiola Emanuel