WATANZANIA KUTIMUA VUMBI LONDON LEO! KUONEKANA MBASHARA DStv







Timu ya Taifa ya Riadha inayoshiriki mashindano ya Dunia ya riadha yanayoendelea jijini London inaanza kibarua cha kuipeperusha bendera yetu leo (Jumamosi 05/08/2017) ambapo mfukuza upepo Failuna Abdi Matanga atakimbia mbio za mita 10,000 leo .


Failuna atashuhudiwa na maelfu ya watanzania kupitia DStv Muda wa saa mbili usiku.

Akithibitisha kuonekana kwa matangazo hayo kupitia DStv, Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande amesema DStv imefanya jitihada kubwa na kuhakikisha kuwa watanzania wanaishuhudia timu yetu ikituwakilisha katika mashindano hayo muhimu ulimwenguni.

“Tunawahakikishia watanzania burudani hii moja kwa moja kupitia DStv chaneli za Supersport. Tunaamini sote tutakuwa nyuma yao wachezaji wetu kuwashuhudia jinsi wanavyotuwakilisha” alisema Maharage

“Suala la watanzania kuwashuhudia vijana wetu wakishiriki katika mashindano makubwa kama haya lina maana kubwa sana. Vijana wadogo wakiwaona dada zao na kaka zao wakishiriki mashindano makubwa kama haya inawatia moyo na kuwapa ari na tamaa ya wao kujitahidi na kufika hatua kama hizo. Hili ni jambo la muhimu sana na sisi DStv tunalitilia mkazo sana. Ni njia moja wapo ya kuwashawishi na kuwatia moyo vijana wetu wanaochipukia na kuwajengea kujiamini”

Baada ya Failuna anayekimbia mita 10,000, watanzania watashuhudia tena shughuli pevu siku ya jumapili kupitia DStv kuanzia majira ya saa nne asubuhi ambapo vidume watatu - Alphonce Felix Simbu, Ezekiel Jafari Ng’imba na Stefano Huche Gwandu watakuwa wakikata upepo katika viunga vya jiji la Malkia London ikiwa ni mbio ndefu za kilomita 42.

Baada ya vidume hao kukamilisha kazi tuliyowatuma, wanawake wetu wa shoka nao wataingia barabarani ambapo Tanzania inawakilishwa na Sara Ramadhani Makera na Magdalena Crispin Shauri ambao nao watafukuza upepo umbali wa kilomita 42 majira ya saa nane mchana. Patashika yote hii itaonekana DStv.

Wanariadha wengine wawili wa mbio fupi za mita 5,000 ambao ni Emmanuel Giniki Gisamoda na Gabriel Gerald Geay watatimka siku ya Jumatano tarehe 9 Agosti majira ya mbili usiku hii ikiwa ni raundi ya mchujo na wakifuzu watashiriki fainali ya mita 5,000 siku ya Jumamosi Agost 12, majira ya mbili usiku. Nao pia watashuhudiwa mbashara kupitia DStv

Mashindano ya Dunia ya Riadha yalianza rasmi 1983 ambapo Tanzania imewahi kupata medali 1 tu ya Fedha kupitia mwanariadha Christopher Isegwe kwenye mbio za Marathon 2005 Helsinki Finland.

Ni mashindano ya pili kwa ukubwa baada ya Olimpiki ambapo nchi 204 zinashiriki mashindano hayo mwaka huu. Tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka huu ndiyo mwaka ambao Tanzania imeleta timu kubwa ya wanariadha 8, ambao ina mchanganyiko wa wanaume na wanawake na pia kuna wakimbiaji wa mbio za uwanjani.
Wanariadha wote wanaoshiriki wamefikia viwango vinavyotakiwa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF)

Post a Comment

0 Comments