Waziri Maghembe 'kuibeba' Rock City Marathon

August 22, 2017





Dar es Salaam;WAZIRI wa Maliasili na Utalii Prof Jumanne Maghembe mwishoni mwa wiki hii alizindua rasmi usajili wa msimu wa nane wa mbio za Rock City Marathon huku akiahidi kushirikiana na waandaaji wa mbio hizo katika kuhakikisha kuwa zinatumika vema kuutangaza utalii wa ndani.


Akizungumza kwenye hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa mchezo huo wakiwemo viongozi wa serikali pamoja na wadhamini mbalimbali wa mbio hizo, Waziri Maghembe alisema azma yake hiyo inasukumwa na malengo ya mbio hizo ambayo ni kutumia mchezo wa riadha katika kutangaza utalii hususani katika Ukanda wa Ziwa.


"Kwa kuzingatia uzito wa malengo ya mbio hizo nitamke bayana kuwa nipo tayari kushirikiana na waandaaji wa mbio hizi kuhakikisha kwamba kuanzia mwaka huu mbio hizi zinafana na zinavutia washiriki wengi zaidi hususani wa kimataifa,'' alisema Waziri Maghembe ambae pia alithibitisha ushiriki wake kwenye mbio hizo zinazoratarajiwa kufanyika Octoba 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na kupita katika barabara mbalimbali za jiji hilo kabla hazijamalizikia katika uwanja huo.


Mbali na ushiriki wake,Waziri Maghembe alitoa wito kwa mashirika mbalimbali yaliyo chini ya wizara yake ikiwemo la Hifadhi za Taifa(Tanapa), Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Makumbusho ya Taifa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kufanikisha mbio hizo.


"Ukanda wa Ziwa una vivutio vingi ambavyo pia kama Wizara yenye dhamana ya utalii lazima tuvigeukie na kuvitangaza kwa nguvu na kwa njia tofauti ikiwemo michezo,'' alisema Waziri Maghembe huku akivitaja baadhi ya vivutio hivyo kuwa ni pamoja na Kisiwa cha Saanane, Makumbusho ya kabila la Wasukuma pamoja na tamaduni za makabila ya wakazi wa Kanda ya Ziwa.


Mbio za Rock City Marathon zilizoanzishwa miaka minane iliyopita zinazozidi kujiongezea umaarufu kila mwaka na tayari zimefanikiwa kuwavutia baadhi ya wadhamini ikiwa ni pamoja na kampuni za TIPER, PUMA, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),Mwanza Hotel , Real PR Solutions Limited, Afrimax Strategic Partnerships Limited, EF Outdoor, CF Hospital na ATCL.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo, Bw Zenno Ngowi alitoa wito kwa washiriki wa ndani hususani wa mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na wadhamini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo ambazo kwa mwaka jana zilifanikiwa kuhusisha washiriki zaidi ya 2000 na watazamaji zaidi ya 30,000.


Naye Mratibu wa mbio hizo zinazoandaliwa na kampuni ya Capital Plus International, Bi Adeline Ndesanjo alisema mbio za mwaka huu zinatarajiwa kuhusisha washiriki wengi zaidi kutoka kila kona ya dunia ikiwemo Afrika, Ulaya,China,Mashariki ya Kati hususani Israel na Marekani huku akitoa wito kwa washiriki wa ndani kujisajili kwa wingi ili kuthibitisha ushiriki wao kwenye mbio hizo.


Akizungumza kwa niaba ya wadhamini wengine wa mbio hizo Meneja Masoko wa Kampuni ya mafuta ya Puma, Bw Machumani Shebe alisema ushiriki wao umechagizwa zaidi na azma ya kampuni hiyo kuisaidia serikali katika kuutangaza utalii wa ndani.


"Tukiwa kama wadau muhimu katika biashara ya mafuta hususani mafuta ya ndege tunategemea sana ustawi wa sekta ya utalii katika kuongeza soko la biashara yetu na kwa kuwa mchezo wa riadha umekuwa ukitumika zaidi katika kuwavutia watalii tukaona kuna haja ya kuunga mkono ufanikishaji wa mbio hizi,'' alisema.




WAZIRI wa Maliasili na Utalii Prof Jumanne Maghembe akizungumza na wadau mbalimbali wa mchezo wa riadha hapa nchini pamoja na waandaaji wa mbio za Rock City Marathon kwenye hafla maalumu ya uzinduzi rasmi usajili wa msimu msimu wa nane wa mbio hizo iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo, Bw Zenno Ngowi akizungumza kwenye hafla hiyo. Alitoa wito kwa washiriki wa ndani hususani wa mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na wadhamini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo ambazo kwa mwaka jana zilifanikiwa kuhusisha washiriki zaidi ya 2000 na watazamaji zaidi ya 30,000.

Mratibu wa mbio hizo zinazoandaliwa na kampuni ya Capital Plus International, Bi Adeline Ndesanjo akitoa maelezo kuhusu maandalizi ya mbio hizo kwenye hafla hiyo. Alisema mbio za mwaka huu zinatarajiwa kuhusisha washiriki wengi zaidi kutoka kila kona ya dunia ikiwemo Afrika, Ulaya,China,Mashariki ya Kati hususani Israel na Marekani .

Wadhamini nao hawakuwa nyuma!Meneja Masoko wa Kampuni ya mafuta ya Puma Energy, Bw Machumani Shebe alisema ushiriki wao kwenye mbio hizo umechagizwa zaidi na azma ya kampuni yake hiyo kuisaidia serikali katika kuutangaza utalii wa ndani.


Baadhi ya wageni waalikwa waliohudhuria hafla hiyo.


WAZIRI wa Maliasili na Utalii Prof Jumanne Maghembe akiwa kwenye picha ya pamoja na waandaaji wa mbio hizo pamoja na wadau mbalimbali wa mchezo huo wakiwemo viongozi wa serikali pamoja na wadhamini wa mbio hizo.

WATANZANIA KUTIMUA VUMBI LONDON LEO! KUONEKANA MBASHARA DStv

August 05, 2017






Timu ya Taifa ya Riadha inayoshiriki mashindano ya Dunia ya riadha yanayoendelea jijini London inaanza kibarua cha kuipeperusha bendera yetu leo (Jumamosi 05/08/2017) ambapo mfukuza upepo Failuna Abdi Matanga atakimbia mbio za mita 10,000 leo .


Failuna atashuhudiwa na maelfu ya watanzania kupitia DStv Muda wa saa mbili usiku.

Akithibitisha kuonekana kwa matangazo hayo kupitia DStv, Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande amesema DStv imefanya jitihada kubwa na kuhakikisha kuwa watanzania wanaishuhudia timu yetu ikituwakilisha katika mashindano hayo muhimu ulimwenguni.

“Tunawahakikishia watanzania burudani hii moja kwa moja kupitia DStv chaneli za Supersport. Tunaamini sote tutakuwa nyuma yao wachezaji wetu kuwashuhudia jinsi wanavyotuwakilisha” alisema Maharage

“Suala la watanzania kuwashuhudia vijana wetu wakishiriki katika mashindano makubwa kama haya lina maana kubwa sana. Vijana wadogo wakiwaona dada zao na kaka zao wakishiriki mashindano makubwa kama haya inawatia moyo na kuwapa ari na tamaa ya wao kujitahidi na kufika hatua kama hizo. Hili ni jambo la muhimu sana na sisi DStv tunalitilia mkazo sana. Ni njia moja wapo ya kuwashawishi na kuwatia moyo vijana wetu wanaochipukia na kuwajengea kujiamini”

Baada ya Failuna anayekimbia mita 10,000, watanzania watashuhudia tena shughuli pevu siku ya jumapili kupitia DStv kuanzia majira ya saa nne asubuhi ambapo vidume watatu - Alphonce Felix Simbu, Ezekiel Jafari Ng’imba na Stefano Huche Gwandu watakuwa wakikata upepo katika viunga vya jiji la Malkia London ikiwa ni mbio ndefu za kilomita 42.

Baada ya vidume hao kukamilisha kazi tuliyowatuma, wanawake wetu wa shoka nao wataingia barabarani ambapo Tanzania inawakilishwa na Sara Ramadhani Makera na Magdalena Crispin Shauri ambao nao watafukuza upepo umbali wa kilomita 42 majira ya saa nane mchana. Patashika yote hii itaonekana DStv.

Wanariadha wengine wawili wa mbio fupi za mita 5,000 ambao ni Emmanuel Giniki Gisamoda na Gabriel Gerald Geay watatimka siku ya Jumatano tarehe 9 Agosti majira ya mbili usiku hii ikiwa ni raundi ya mchujo na wakifuzu watashiriki fainali ya mita 5,000 siku ya Jumamosi Agost 12, majira ya mbili usiku. Nao pia watashuhudiwa mbashara kupitia DStv

Mashindano ya Dunia ya Riadha yalianza rasmi 1983 ambapo Tanzania imewahi kupata medali 1 tu ya Fedha kupitia mwanariadha Christopher Isegwe kwenye mbio za Marathon 2005 Helsinki Finland.

Ni mashindano ya pili kwa ukubwa baada ya Olimpiki ambapo nchi 204 zinashiriki mashindano hayo mwaka huu. Tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka huu ndiyo mwaka ambao Tanzania imeleta timu kubwa ya wanariadha 8, ambao ina mchanganyiko wa wanaume na wanawake na pia kuna wakimbiaji wa mbio za uwanjani.
Wanariadha wote wanaoshiriki wamefikia viwango vinavyotakiwa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF)
 

Copyright © 2015 - 2025 Athletics Tanzania All Right Reserved

Developed by Gadiola Emanuel
Theme By AP | Developed By Gadiola Emanuel