RT YAWATAKA WATAALAM WA RIADHA NCHINI KUWASILISHA TAARIFA ZAO

February 05, 2023

 





NA TULLO CHAMBO, RT

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limewataka wataalamu wote wa mchezo huo kuwasilisha taarifa zinazoonyesha fani zao.
Agizo hilo, limetolewa na Kaimu Katibu Mkuu RT, Wakili Jackson Ndaweka, ambako amewataka makatibu wa vyama vya riadha mikoa yote ya Tanzania Bara, kuwajulisha wataalam wa riadha waliopo mikoani mwao, kuwasilisha taarifa zinazoonyesha fani zao katika mchezo huo. 

Wakili Ndaweka,amesema RT inakusudia kuendesha kozi mbalimbali za kuboresha uwezo wa wataalamu wa mchezo wa riadha waliopo na kuzalisha wengine katika fani ambazo zina upungufu. 

"Ili mpango huu uweze kutekelezeka kwa ufanisi, ni lazima kuwa na taarifa za wataalamu wa Riadha nchini, zitakazowezesha kuainisha maeneo yenye upungufu na kuyawekea mpango maalum," alisema na kufafanua. 

Taarifa zinazotakiwa zinapaswa kuwasilishwa kupitia wasifu 'CV', ambayo inapaswa kuambatanishwa na vivuli vya vyeti vya elimu ya Riadha na elimu ya kawaida. 

Wakili Ndaweka, alisema takwimu hizo ni muhimu sana kwa maendeleo ya mchezo wa riadha nchini. 

"Makatibu wanapaswa kuwajulisha wataalam waliopo kwenye mikoa yao, wawasilishe taarifa hizo kupitia anuani ya barua pepe ya shirikisho ambayo ni tan@mf.worldathletics.org si zaidi ya tarehe 20/02/2023," alisisitiza Ndaweka.

RT YAANIKA MATUKIO MANNE MAKUBWA YA KIMATAIFA 2023

February 04, 2023

 


| Yataka ushirikiano, uwajibikaji ngazi zote

|Timu ya Cross Country kuagwa Februari 14

NA TULLO CHAMBO, RT

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limeanika matukio manne makubwa ya kimataifa yanayolikabili mwaka 2023 na kusisitiza uwajibikaji wa pamoja kwa ngazi zote ili kuleta matokeo chanya.

Akizungumza na Wanahabari jijini Mwanza Februari 3, Rais wa RT, Silas Lucas Isangi, ameyataja matukio hayo ni Mashindano ya Mbio za Nyika 'Cross Country' ya Dunia, Bathurst, Australia Februari 18, Mashindano ya Vijana Afrika Mashariki (EAAR), U 18 na 20 Tanzania itakuwa mwenyeji Machi 10-11.

Tukio la tatu, Isangi alitaja ni Mashindano ya Afrika U 18 na 20 Lusaka Zambia  Aprili 27 hadi Mei 3.

"Pia kuna mashindano ya Common Wealth U 18 huko Trinidad na Tobago Agosti 4-11, vile vile All Africa Games Julai 4-23 nchini Ghana na Mashindano ya Dunia Budapest, Hungary" alisema na kuongeza.

Kwa kifupi mwaka huu uko bize sana, hivyo viongozi wa Riadha ngazi za chini kabisa, lazima wote tuamke na kutimiza wajibu kwa vitendo.

Rais Isangi, aliitaka mikoa yote ifanye mashindano ya vijana ili kufanikisha upatikanaji wa timu ya Taifa U 18 na 20 yenye tija. Pia ushiriki wao kwenye mashindano ya Taifa uwe wenye tija.

TIMU YA TAIFA CROSS COUNTRY
Rais Isangi, amesema timu hiyo imeanza kambi toka Februari Mosi katika Hoteli ya Mvono, Ngaramtoni jijini Arusha kwa gharama za shirikisho asilimia 100.

Amesema, timu itakaa kambini hadi Februari 12, itakapokwenda jijini Dar es Salaam tayari kwa kuagwa Februari 14, kabla ya kukwea pipa kwa safari ya Australia.

Amesema timu hiyo itakuwa chini ya Kiongozi wa msafara, Wakili Jackson Ndaweka ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu RT, Kocha Denis Male, huku wachezaji ni Mathayo Sombi, Inyasi Sulle, Fabian Nelson na Josephat Gisemo.

"Maandalizi yote yamekamilika ikiwamo tiketi, visa na vibali vyote vya serikali vimekamilika," alisema na kuishukuru serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kwa kusaidia katika maandalizi hayo.
 

Copyright © 2015 - 2025 Athletics Tanzania All Right Reserved

Developed by Gadiola Emanuel
Theme By AP | Developed By Gadiola Emanuel