Kutoka Kulia: Ofisa wa BMT Charles Maguzu, Makamu wa Rais William Kallaghe na Mjumbe wa Kanda ya Kaskazini Alfredo Shahanga.
NA TULLO CHAMBO, RT
BAADA ya kutokea sintofahamu ya muda mrefu kati ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), na waandaaji wa matukio mbalimbali ya mbio za barabarani (RO's), hatimaye imefikia tamati.
Tamati hiyo imefikiwa baada ya kikao cha pamoja kati ya RT, RO's na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Machi 4 mwaka huu.
Katika kikao hicho kilichokuwa chini ya Makamu wa Rais wa RT , William Kallaghe na Ofisa Michezo BMT, Charles Maguzu, kilijadili kwa kina changamoto zinazokabili pande zote tatu.
Baada ya majadiliano ya takribani saa sitaa, pande zote zilipitia vifungu mbalimbali vya kikanuni na kuafikiana kuziheshimu ili kujenga ustawi bora wa mchezo wa riadha nchini.
Kikubwa kilichokaziwa, ni waandaaji kuheshimu mamlaka zilizopo na mamlaka kutenda haki kwa wateja wao (RO's).
Kikubwa Makamu wa Rais wa RT, Kallaghe aliwataka waandaaji kuheshimu na kushirikiana vyema na vyama vya riadha vya mikoa, na kwamba kuanzia hivi sasa waandaaji wanatakiwa kupata baraka za vyama vya mikoa kabla ya kuanza kutangaza matukio yao.
0 Comments