Usajili Azania Kids Run 2016 wapamba moto

June 02, 2016


MCHAKATO wa usajili wa washiriki wa Mbio za Watoto za Azania Bank Kids Run 2016, umezidi kushika kasi, huku siku tatu zikiwa zimesalia kabla ya kufanyika kwake Juni 5 kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, mmoja wa waratibu wa mbio hizo, Wilhelm Gidabuday, alisema kufikia jana mchana, mchakato wa usajili ulikuwa ukiendelea vema, ambako wazazi na walezi wamejitokeza kusajili watoto wao.

Gidabuday alisema kuwa, matarajio ni kusajili watoto wapatao 2,000 walio na umri chini ya miaka 16, ambao watashiriki Azania Bank Kids Run 2016, mbio zilizogawanywa katika kategori tano za kilomoita 5, km 2, km 1, mita 100 na mita 50.
Alibainisha kuwa, fomu za ushiriki zinapatikana katika Matawi ya Azania Bank popote jijini Dar es Salaam, pamoja na Ofisi za Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), pamoja na Ofisi za BMT zilizoko Samora Avenue katikati ya jiji. Aliwataka wazazi na walezi ambao hawajachukua fomu za ushiriki wa watoto wao, kuchangamkia mchakato huo kwa kufika katika vituo husika na kununua fomu hizo kwa shilingi 2,000 tu, ili kuwawezesha watoto kushiriki na kushinda zawadi.

Naye, Ofisa Masoko Mwandamizi wa Azania Bank inayodhamini mashindano hayo, Othman Jibrea, alisisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kusajili watoto wao katika Azania Bank Kids Run, ili kufikia lengo lao la kuibua vipaji vipya vya riadha.

Jibrea alibainsiha kuwa, Azania Bank imejitosa kudhamini mbio hizo kutokana na mlengo wake wa kuibua vipaji vichanga katika riadha, hivyo ili kufikia lengo, wazazui na walezi hawana budi kujitokeza kwa wingi kusajili watoto wao.

Alizitaja zawadi za mbio za Kilomita tano kuwa ni Sh. 200,000 kwa mshindi wa kwanza, Sh. 150,000 kwa mshindi wa pili na Sh. 100,000 kwa mshindi wa tatu, wote wakitarajiwa pia kupata medali, begi lenye vifaa vya shule na sare za michezo (track suit).

Jibrea alibainisha kuwa, mshindi wa kwanza wa mbio za kilomita 2 atajinyakulia Sh. 100,000, mshindi wa pili Sh. 75,000 na mshindi wa tatu Sh. 50,000, pamoja na medali, begi lenye vifaa vya shule na sare za michezo.

Katika mbio za kilomita 1, Jibrea alitaja zawadi za washindi kuwa ni Sh. 75,000 kwa mshindi wa kwanza, 50,000 kwa mshindi wa pili na Sh. 40,000 kwa wa tatu, ambao watapata zawadi ya ziada ya medali, begi lenye vifaa vya shule na sare za michezo.

"Pia, washindi wa nne hadi wa 10 wa mbio hizo, watapata kifuta jasho cha Sh. 15,000, begi lenye vifaa vya shule na sare za michezo. Nia ni kuwafanya watoto watakaoshiriki kutotoka bure mwishoni mwa mashindano," alisema Jibrea.

RT, Azania Bank watangaza zawadi za Kids Run zitakazofanyika Mei 5 kwenye viwanja vya mnazi mmoja kutumia Sh. Milioni 130 na ushee

June 01, 2016


Ofisa Masoko Mwandamizi wa benki ya Azani, Othman Jibrea(kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo katika Ofisi za Baraza la Michezo la Taifa (BMT). Kulia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya RT, Tullo Chambo.

Na Mwandishi Wetu
RIADHA Tanzania (RT) kwa kushirikiana na Benki ya Azani, leo wametangaza zawadi kwa washindi wa mbio za watoto, Kids Run, zitakazofanyika Juni 5 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya RT, Tullo Chambo alisema  mbio hizo zitakuwa katika vipengele vitano vya umbali wa kilometa tano, mbili na moja, huku zingine ni meta 100 na meta 50 kwa wavulana na wasichana kulingana na umri.
 
Alisema wale wa kilometa tano, mbili na moja wenyewe watapita katika barabara mbalimbali za jijini Dar es Salaam na kumalizia mbio hizo katika viwanja hivyo vya Mnazi Mmoja walikoanzia.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Riadha Tanzania (RT), Tullo Chambo akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu Kids Run zitakazofanyika Mei 5 jijini Dar es Salaam.
Alisema maandalizi yanaenda vizuri na ni matarajio yao kuwa zaidi ya watoto 2,000 watajitokeza kushiriki katika mbio hizo za kwanza na aina yake kushirikisha watoto.

Ofisa Masoko Mwandamizi wa benki ya Azani, Othman Jibrea alisema kuwa mshindi wa kwanza wa mbio za kilometa tano ataondoka na sh. 200,000, suti ya michezo na vifaa vya shule.

Mratibu wa Kids Run, Wilhelm Gidabuday akizungumza leo kuhusu mbio hizo. Kulia ni Ofisa Masoko Mwandamizi wa Benki ya Azania, Othman Jibrea.
Mshindi wa pili atapewa sh. 150,000 suti ya michezo na vifaa vya elimu, wakati mshindi watatu atapewa sh. 100,000 na vifaa vya elimu.

Mshindi wa kwanza katika mbio za kilometa mbili ataondoka n ash. 100,000, wakati wa pili atapewa sh. 75,000 na watatu sh. 50,000, ambapo wote mbali na zawadi za fedha watapewa vifaa vya shule.
 
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Riadha Tanzania, RT, Tullo Chambo.
Jibrea alisema washindi wa kilometa moja watapata zawadi za sh. 75,000, 50,000 na 40,000 pamoja na vifaa vya shule.
Alisema kuwa washindi wote pia watafungiliwa akaunti katika benki ya Azani, ambako watawekewa zawadi zao hizo.

Aidha, Benki ya Azani imesema kuwa itatumia zaidi ya Sh.Milioni 130 kugharamia mashindano hayo, ambayo ni ya kwanza na ya aina yake kufanyika hapa nchini.
Ofisa Masoko Mwandamizi wa benki ya Azani, Othman Jibrea akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu Kids Run.
 Watoto wa umri tofauti wanatarajia kuchuana vikali katika mbio hizo za Kids Run Mei 5, 2016.
 

Copyright © 2015 - 2025 Athletics Tanzania All Right Reserved

Developed by Gadiola Emanuel
Theme By AP | Developed By Gadiola Emanuel