RT YAUONGEZEA THAMANI UWANJA WA BENJAMIN MKAPA, DAR

March 12, 2023

 







 NA TULLO CHAMBO, RT


SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), kwa ushirikiano na shirikisho la mchezo huo nchini Kenya (AK), wamezindua kifaa maalum cha kupima hali ya hewa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kifaa hicho ni maalumu kwa ajili ya kupima ubora wa hali ya hewa sehemu husika, kama iko sawa kwa matumizi ya wanamichezo shiriki wakati wa tukio ama haiko sawa.

Ufungaji wa kifaa hicho ni maagizo ya Shirikisho la Riadha la Kimataifa (WA), ambapo Tanzania imekuwa nchi ya nne barani Afrika kupata teknolojia hiyo. 

Akizungumza  wakati wa uzinduzi huo mbele ya Mgeni rasmi Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, Rais wa AK ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Riadha Ukanda wa Afrika Mashariki (EAAR), Luteni Jenerali mstaafu Jackson Tuwei, alisema kifaa hicho ni muhimu kwani binadamu hata wanyama wanahitaji kuishi katika mazingira ya hali ya hewa safi.

Luteni Jenelari Tuwei, alisema teknolojia hiyo imeanza kutumika nchini Kenya, kisha ilifuatiwa na Dakar Senegal, Addis Ababa Ethiopia na Tanzania imekuwa ni nchi ya nne kufungwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na badae wanatarajia kufunga kifaa hicho nchini Zambia ambako yanatarajiwa kufanyika mashindano ya vijana Afrika Aprili 27 hadi Mei 3.

Kwa upande wake, Katibu wa BMT, Neema Msitha, alishukuru kwa jambo hilo ambalo linauongezea thamani wa Uwanja wa Benjamin Mkapa kimataifa, na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, mbali ya kuipongeza RT kwa kufanikisha jambo hilo lenye manufaa kwa wanamichezo wote watakaokuwa wanautumia uwanja huo, iko tayari kutoa Ushirikiano katika kila  jambo lenye maendeleo kwenye sekta ya michezo na kwamba wadau wote wa michezo wanakaribishwa.

Kifaa hicho kimetengenezwa na taasisi ya mazingira nchini Sweden ijulikanayo kama Stocklohom Environment Instute (SEI).

SASA RIADHA NA WAANDAAJI " RACE ORGANIZERS" DAM DAM

March 05, 2023

 

Kutoka Kulia: Ofisa wa BMT Charles Maguzu, Makamu wa Rais William Kallaghe na Mjumbe wa Kanda ya Kaskazini Alfredo Shahanga.


NA TULLO CHAMBO, RT

BAADA ya kutokea sintofahamu ya muda mrefu kati ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), na waandaaji wa matukio mbalimbali ya mbio za barabarani (RO's), hatimaye imefikia tamati.

Tamati hiyo imefikiwa baada ya kikao cha pamoja kati ya RT, RO's na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Machi 4 mwaka huu.
Katika kikao hicho kilichokuwa chini ya Makamu wa Rais wa RT , William Kallaghe na Ofisa Michezo BMT, Charles Maguzu, kilijadili kwa kina changamoto zinazokabili pande zote tatu.
Baada ya majadiliano ya takribani saa sitaa, pande zote zilipitia vifungu mbalimbali vya kikanuni na kuafikiana kuziheshimu ili kujenga ustawi bora wa mchezo wa riadha nchini.

Kikubwa kilichokaziwa, ni waandaaji kuheshimu mamlaka zilizopo na mamlaka kutenda haki kwa wateja wao (RO's).
Kikubwa Makamu wa Rais wa RT, Kallaghe aliwataka waandaaji kuheshimu na kushirikiana vyema na vyama vya riadha vya mikoa, na kwamba kuanzia hivi sasa waandaaji wanatakiwa kupata baraka za vyama vya mikoa kabla ya kuanza kutangaza matukio yao.

19 WAPENYA TIMU YA TAIFA VIJANA EAAR

March 05, 2023


Wanariadha wakichuana kwenye mashindano ya Majaribio Jijini Dar es Salaam.

Makamu wa rais wa shirikisho la Riadha la Tanzania, Ndugu William Kallaghe akizungumza na wanariadha waliopenya kwenye timu ya Taifa ya Vijana ya EAAR Dar es Salaam.


NA TULLO CHAMBO, RT

WANARIADHA 19 wamefanikiwa kuchaguliwa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 18 na 20 itakayoiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Afrika Mashariki (EAAR U 18 & U 20 yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, kuanzia Machi 9 mwaka huu.
Wanariadha hao wamepatikana kupitia mashindano ya wazi ya Taifa, yaliyofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es  Salaam Machi 4 mwaka huu, ambayo yaliandaliwa na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).

Jopo la Wataalamu wakiongozwa na Makocha wa Taifa wa timu hiyo, Robert Kalyahe na Mwinga Mwanjala, lilichagua wanariadha hao kutokana na viwango ambavyo wanariadha hao walivionyesha na si kutokana na nafasi walizoshika katika mchezo husika.

Aidha makocha hao, walibainisha kuwa wameshuhudia vipaji vipya vingi wameviona na kama vikiendelezwa vitakuja kuwa lulu kwa Taifa siku zijazo.
Kutokana na vijana hao 19 waliofuzu, wengine nane watajumuishwa nao ambao walifanya vema katika mashindano mengineyo ikiwemo Ladies First yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada kutangazwa timu hiyo mbele ya viongozi wa mikoa iliyoshiriki Tabora, Mbeya, Pwani, Dar es Salaam, Arusha, Morogoro, makocha mbalimbali na Waandaaji wa Matukio ya Riadha 'Race Organizers' (RO's), Makamu wa Rais wa RT, William Kallaghe, aliwapongeza wote waliofanikisha tukio hilo na kubainisha kwamba, kati ya malengo makuu ya shirikisho hivi sasa ni kuwekeza kwa vijana ambao ndio hazina ya kesho ya Taifa.

"Kati ya mikakati mikubwa hivi sasa ya RT ni kwenye mbio za uwanjani....Na hakuna ujanja bali kuwekeza kwa vijana na ndio maana tunawaomba na kuwahimiza wadau kusapoti katika hili.
"Vijana hawa tuliowapata ndo tunaanza nao, hivyo tunawaomba wadau mbalimbali mtuunge mkono katika hili kwa manufaa ya Taifa siku zijazo, na ambao hamkufanikiwa kuingia katika timu hii, msikate tamaa kwani bado nafasi mnayo mzidishe juhudi," alisema Kallaghe na kuongeza.

Timu hiyo itaingia kambini mapema Jumatatu kwenye hosteli za Baraza la Maaskofu (TEC), Kurasini jijini Dar es Salaam.
Wanariadha 19 waliopenya ni pamoja na Siwema Julias, Shija Donald, Salma Samwel, Christina George, Elizabeth Kirario,     Bravo George, Kimena Kibase, Damian Christian, Fedelis Amadi, Baraka Tiluli na Emmanuel Amos.

Wengine ni Elizabeth Ilanda, Gaudensia Maneno, Elia Clement, Nicodemus Joseph, Nelson Mangura, Jackson Sylvester, Dickson Mangura na Malcolm Kazmir.

RT YATEKELEZA MAAGIZO YA BMT

March 05, 2023

 

Kulia ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania RT , Ndugu William Kallaghe akikabidhi ripoti kwa Katibu Mkuu Mtendaji wa BMT, Bi. Neema Msitha Jijini Dar es Salaam.


SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), Machi 3, 2022, limetekeleza agizo la Baraza la Michezo la Taifa (BMT), baada ya kukabidhi ripoti ya mapato na matumizi.

Ripoti hiyo imekabidhiwa na Makamu wa Rais wa RT, William Kallaghe, kwa Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha.
BMT ilifanya kikao na Kamati ya Utendaji ya RT,    Januari 21 kwenye moja ya kumbi za Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, na moja ya maelekezo ya Baraza, ilikuwa ni kuitaka RT kuwasilisha ripoti ya mapato na matumizi 2020/21 hadi 2021/22.

Baada ya kuipokea ripoti hiyo, Katibu Mtendaji BMT, Msitha, alisema watakaa na kuifanyia kazi.
 

Copyright © 2015 - 2025 Athletics Tanzania All Right Reserved

Developed by Gadiola Emanuel
Theme By AP | Developed By Gadiola Emanuel