Showing posts with label Events. Show all posts
Showing posts with label Events. Show all posts

ROGATH JOHN STEPHEN AKHWARI ACHAGULIWA KUWA RAIS WA SHIRIKISHO LA RIADHA TANZANIA

August 17, 2025

 

Kocha wa Polisi Tanzania na Katibu Mkuu wa Riadha Chama cha Mkoa wa Arusha Rogath John Stephen Akhwari amechaguliwa na wajumbe kuwa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania huko Mwanza tarehe 16/08/2025 kwa kupata Kura 27 kati ya 47 na mpinzani wake Bw. Nsolo Malongo Mlozi kupata kura 20. 
Wakili Jackson Beda Ndaweka Achaguliwa kuwa Makamu wa Shirikisho la Riadha Tanzania -RT , baada ya kuitumikia shirikisho la riadha Tanzania kama Kaimu Katibu Mkuu kwa Muda mrefu.

JACKLINE SAKILU ASHINDA MBIO ZA CHONGQING INTERNATIONAL MARATHON, CHINA

March 24, 2024

 

Jackline Sakilu (TAN) competing in the women's marathon on day two of the Commonwealth Games at Cannon Hill Park, Edgbaston in Birmingham, England, on July 30, 2022. Credit : Gary Mitchell-GMP Media


Mwanariadha wa Kimataifa wa Mbio ndefu (Marathon) Jackline Juma Sakilu ashinda mbio za Chongqing International Marathon, China kwa kuwa wa kwanza kwa muda wa saa mbili na dakika ishirini na moja na sekunde ishirini na sita (02:21:26) leo tarehe 24/03/2024 na kuchukua medali ya Dahahabu.

Jackline Sakilu, amefuzu na wenzake 3 kushiriki mashindano makubwa ya olimpiki Jijini Paris, Ufaransa, wenzake waliofuzu kwa mashindano hayo ni Alphonce Felix Simbu, Gabriel Gerald Geay na Magdalena Crispine Shauri.

Tunampongeza Jackline Sakilu kwa Ushindi huo.

Mwanariadha Andrew Rhobi amepata muda wake Bora

March 10, 2024

 

Copyright @gettyimages

Hongera kwa Andrew Boniface Rhobi kutoka jeshi la polisi Tanzania kwa kupata muda wako bora wa dakika tatu na sekunde hamsini na moja ( 3:51.44) yaani ( Personal Best) mita 1500 (1500M) na kuwa nafasi ya Saba kwenye heat ya kwanza, kwenye Mashindano ya Dunia ya Ndani ( World Athletics indoors Championships Glasgow 2024) tarehe 1-3 Machi 2024, huko Glasgow, Scotland.

GEAY 'AKICHAFUA' MBEYA TULIA MARATHON 2023

May 06, 2023


 

BINGWA wa Taifa anayeshikilia rekodi ya Marathon Tanzania, Gabriel Gerald Geay amekuwa kivutio kikubwa Mbeya Tulia Marathon, aliposhiriki na kuibuka mshindi katika mbio za mita 1500.

Mbeya Tulia Marathon, imekata utepe Leo Mei 5 kwa mbio za uwanjani, kabla ya kesho Jumamosi Mei 6 kurindima Marathon.

Katika mbio hizo za mita 1500, Geay alianza taratibu raundi ya kwanza akiwa nyuma, kabla ya mzunguko wa pili kupata dhoruba la kuangushwa, lakini alinyanyuka na kukiwasha na hatimaye kuibuka mshindi akitumia dakika 3:58.46.

Geay alifuatiwa na Faraja Damas wa JWTZ aliyetumia dakika 4:00.08 huku nafasi ya tatu ikienda kwa John Joseph pia JWTZ 4:06.25. 

Mashabiki na viongozi mbalimbali waliojitokeza, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa, walishindwa kujizua kumshangilia Geay wakati akikiwasha katika mbio hizo.

Kwa upande wa wanawake Mita 1500, Magdalena Shauri wa JWTZ, alishinda akitumia dakika 4:31.13 na kufuatiwa na Salma Charles ambaye katoka Zambia na Timu ya Taifa U 18 na 20 iliyoshiriki mashindano ya Afrika, dakika 4:46.55 na wa tatu akiwa ni Mayselina Mbua JWTZ 4:53.16.

Mbali na Geay ambaye katoka kufanya kweli katika mbio kongwe za Boston Marathon nchini Marekani alikoshika nafasi ya pili hivi karibuni, pia mkali mwingine, ambaye pia ni Mshindi wa medali ya Fedha Jumuiya na Mwanamichezo Bora Tuzo za BMT 2022, Alphonce Simbu, naye alikuwepo kushuhudia mbio hizo.

Pia, Timu ya Taifa ya Vijana iliyopumzika hapa ikitokea Ndola Zambia ilikojinyakulia medali mbili katika mashindano ya Afrika, baadhi walipata nafasi ya kushiriki mbio za uwanjani Mbeya Tulia Marathon.

Timu hiyo inatarajiwa kuondoka Mbeya kesho Jumapili kurejea Dar es Salaam.

Pia, mbio hizo zilipambwa program ya watoto 'Kids Athletics', ambayo ilikuwa kivutio kwa watoto wa shule za msingi walioshiriki.

JK AKUTANA NA MWANARIADHA WA KIMATAIFA GABRIEL GERALD GEAY BOSTON, MAREKANI

April 19, 2023

 Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na wanariadha Gabriel Geay (kushoto kwake) na Wence Tarimo (kulia kwake) ambao walishiriki katika Mashindano ya Riadha yaliyofanyika Boston, Marekani tarehe 17 Aprili 2023, ambapo Geay aliibuka mshindi wa pili. Kulia ni Mhe. Saada Mkuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Fedha na Uchumi - wa Zanzibar.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akipokea zawadi ya jezi toka kwa mhamasishaji mashuhuri Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo wakati alipoonana na wanariadha Gabriel Geay (kushoto kwake) na Wence Tarimo (kulia kwake) ambao walishiriki katika Mashindano ya Riadha yaliyofanyika Boston, Marekani tarehe 17 Aprili 2023, ambapo Geay aliibuka mshindi wa pili. Kulia ni Mhe. Saada Mkuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Fedha na Uchumi - wa Zanzibar.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini kwenye kitabu cha mwanariadha Gabriel Geay mjini Boston Marekani, siku moja baada ya shujaa huyo kushika nafasi ya pili kwenye mbio za Boston Marathon.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na wanariadha Gabriel Geay (kushoto kwake) na Wence Tarimo (kulia kwake) ambao walishiriki katika Mashindano ya Riadha yaliyofanyika Boston, Marekani tarehe 17 Aprili 2023, ambapo Geay aliibuka mshindi wa pili. Kulia ni Mhe. Saada Mkuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Fedha na Uchumi - wa Zanzibar na kushoto ni mhamasishaji mashuhuri Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mhe. Saada Mkuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Fedha na Uchumi - wa Zanzibar wakiwa na Watanzania waishio Marekani pamoja na wanariadha Gabriel Geay na Wence Tarimo ambao walishiriki katika Mashindano ya Riadha yaliyofanyika Boston, Marekani tarehe 17 Aprili 2023, ambapo Geay aliibuka mshindi wa pili. Kulia ni mhamasishaji mashuhuri Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo na kushoto ni mtoto wa Bongo Zozo.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi kitabu mwanariadha Gabriel Geay mjini Boston Marekani, siku moja baada ya shujaa huyo kushika nafasi ya pili kwenye mbio za Boston Marathon.

*******

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekutana na Wanariadha Gabriel Geay na Wence Tarimo walioshiriki katika Mashindano ya Marathon yaliyofanyika Boston, Marekani tarehe 17 Aprili 2023.

Gabriel Geay aliibuka mshindi wa pili katika mashindano hayo. Mheshimiwa Rais Mstaafu amempongeza Gabriel Geay kwa ushindi mkubwa na kwa kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Pamoja na wanariadha hao, walikuwepo pia wahamasishaji mbalimbali akiwemo “Bongo Zozo”. Amewapongeza pia kwa kuhamasisha ushindi huu na kufanikisha kuinua bendera ya Tanzania juu.

Mheshimiwa Rais Mstaafu yuko Boston, Marekani ambapo anashiriki katika kutoa mafunzo kwa Mawaziri wa Fedha kutoka nchi mbalimbali zinazoendelea kupitia Mpango wa Uongozi wa Harvard “Harvard Ministerial Leadership Program”.

Katika mafunzo hayo, Mhe. Saada Mkuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Fedha na Uchumi - wa Zanzibar ameshiriki pia.

RT YAUONGEZEA THAMANI UWANJA WA BENJAMIN MKAPA, DAR

March 12, 2023

 







 NA TULLO CHAMBO, RT


SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), kwa ushirikiano na shirikisho la mchezo huo nchini Kenya (AK), wamezindua kifaa maalum cha kupima hali ya hewa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kifaa hicho ni maalumu kwa ajili ya kupima ubora wa hali ya hewa sehemu husika, kama iko sawa kwa matumizi ya wanamichezo shiriki wakati wa tukio ama haiko sawa.

Ufungaji wa kifaa hicho ni maagizo ya Shirikisho la Riadha la Kimataifa (WA), ambapo Tanzania imekuwa nchi ya nne barani Afrika kupata teknolojia hiyo. 

Akizungumza  wakati wa uzinduzi huo mbele ya Mgeni rasmi Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, Rais wa AK ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Riadha Ukanda wa Afrika Mashariki (EAAR), Luteni Jenerali mstaafu Jackson Tuwei, alisema kifaa hicho ni muhimu kwani binadamu hata wanyama wanahitaji kuishi katika mazingira ya hali ya hewa safi.

Luteni Jenelari Tuwei, alisema teknolojia hiyo imeanza kutumika nchini Kenya, kisha ilifuatiwa na Dakar Senegal, Addis Ababa Ethiopia na Tanzania imekuwa ni nchi ya nne kufungwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na badae wanatarajia kufunga kifaa hicho nchini Zambia ambako yanatarajiwa kufanyika mashindano ya vijana Afrika Aprili 27 hadi Mei 3.

Kwa upande wake, Katibu wa BMT, Neema Msitha, alishukuru kwa jambo hilo ambalo linauongezea thamani wa Uwanja wa Benjamin Mkapa kimataifa, na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, mbali ya kuipongeza RT kwa kufanikisha jambo hilo lenye manufaa kwa wanamichezo wote watakaokuwa wanautumia uwanja huo, iko tayari kutoa Ushirikiano katika kila  jambo lenye maendeleo kwenye sekta ya michezo na kwamba wadau wote wa michezo wanakaribishwa.

Kifaa hicho kimetengenezwa na taasisi ya mazingira nchini Sweden ijulikanayo kama Stocklohom Environment Instute (SEI).

SASA RIADHA NA WAANDAAJI " RACE ORGANIZERS" DAM DAM

March 05, 2023

 

Kutoka Kulia: Ofisa wa BMT Charles Maguzu, Makamu wa Rais William Kallaghe na Mjumbe wa Kanda ya Kaskazini Alfredo Shahanga.


NA TULLO CHAMBO, RT

BAADA ya kutokea sintofahamu ya muda mrefu kati ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), na waandaaji wa matukio mbalimbali ya mbio za barabarani (RO's), hatimaye imefikia tamati.

Tamati hiyo imefikiwa baada ya kikao cha pamoja kati ya RT, RO's na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Machi 4 mwaka huu.
Katika kikao hicho kilichokuwa chini ya Makamu wa Rais wa RT , William Kallaghe na Ofisa Michezo BMT, Charles Maguzu, kilijadili kwa kina changamoto zinazokabili pande zote tatu.
Baada ya majadiliano ya takribani saa sitaa, pande zote zilipitia vifungu mbalimbali vya kikanuni na kuafikiana kuziheshimu ili kujenga ustawi bora wa mchezo wa riadha nchini.

Kikubwa kilichokaziwa, ni waandaaji kuheshimu mamlaka zilizopo na mamlaka kutenda haki kwa wateja wao (RO's).
Kikubwa Makamu wa Rais wa RT, Kallaghe aliwataka waandaaji kuheshimu na kushirikiana vyema na vyama vya riadha vya mikoa, na kwamba kuanzia hivi sasa waandaaji wanatakiwa kupata baraka za vyama vya mikoa kabla ya kuanza kutangaza matukio yao.

 

Copyright © 2015 - 2025 Athletics Tanzania All Right Reserved

Developed by Gadiola Emanuel
Theme By AP | Developed By Gadiola Emanuel