Showing posts with label Kitaifa. Show all posts
Showing posts with label Kitaifa. Show all posts

Matukio Mbalimbali ya Mashindano ya Riadha kwa wanawake " Ladies First 2025 " yanayofanyika katika Uwanja wa Benjamin mkapa.

November 30, 2025

 



























Matukio mbalimbali ya mashindano ya riadha kwa wanawake " Ladies First 2025 " yanayofanyika katika Uwanja wa Benjamin mkapa. #AthleticsTanzania

Washindi NBC Dodoma Marathon Kuiwakilisha Tanzania Kimataifa, Dkt Ndumbaro Athibitisha Ushiriki Wake Mbio Za Km 42

July 23, 2024

Serikali imesisitiz dhamira yake ya kutumia mbio za NBC Dodoma Marathon kama chanzo cha kuwapata wanariadha sahihi watakaoliwakilisha taifa kwenye mashindano ya kimataifa yakiwemo mashindano ya Olympic na Mashindano ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth).  Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Damas Ndumbaro amebainisha dhamira hiyo ya serikali jijini Dar es Salaam leo huku akithibitisha nia yake ya kukimbia km 42 (full marathon) kwenye mbio hizo zinatotarajiwa kufanyika jijini Dodoma, Julai 28 mwaka huu. 

Lengo kuu la mbio hizo zinazotarajiwa kuongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ni kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na  kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga  ili kuboresha afya ya mama wa mtoto.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya benki ya NBC  akiwa sambamba na mwenyeji wake Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw Theobald Sabi,  Dkt Ndumbaro pamoja na kusifia jitihada za benki hiyo katika kuinua sekta ya michezo nchini, alisema kwasasa taifa linakabiliwa na uhaba mkubwa wa wanariadha wenye sifa ya kushiriki mashindano ya kimataifa hivyo serikali imejipanga kutumia mbio hizo kutambua wanariadha wenye sifa sahihi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano mbalimbali ya kimataifa.

“Kwasasa kwenye mashindano ya Olympic tunakwenda na wanariadha wachache sana kwasababu hatuna maandalizi ya kutosha. Hivyo NBC Dodoma Marathon ni moja ya chanzo cha kupata wanariadha wazuri ili baada ya mbio hizi tuweze kuwatamuba na kuwapa mafunzo zaidi ili mashindano ya ‘Commonwealth’ na Olympic na mengine mbalimbali ya kimataifa tuwe na wanariadha wengi zaidi.’’ Alibainisha Dkt. Ndumbaro huku akipongeza maandalizi ya mbio yenye kuzingatia viwango vya kimataifa.

Aidha Dkt. Ndumbaro aliipongeza benki hiyo kwa jitihada mbalimbali za kuendeleza sekta ya utamaduni, sana ana michezo kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo udhamini wa michezo na huduma za kibenki zinazolenga kuwasaidia wadau mbalimbali wa sekta hizo.

Tofauti na mbio hizi, jitihada za benki ya NBC kwenye kuinua sekta ya michezo zinaonekana kupitia udhamini wake kwenye ligi za NBC Premier League, NBC Championship na NBC Youth league ambapo imewekeza kiasi cha Sh.32.6 Bilioni kwenye ligi hizo. Pia benki hii ina inashiriki katika uwezeshaji kiuchumi kwa wasanii kupitia mfuko wa maendeleo ya sanaa nchini sambamba na kusimamia kamati ya Hamasa ya Timu za Taifa ambapo mpaka sasa imeshakusanya kiasi cha Shilingi 2 bilioni kati kutokana na ahadi za awali za Sh.4 bilioni zilizopokelewa katika hafla ya uzinduzi wa kamati hiyo,’’ alisema.

Awali akizungumza kwenye mkutano huo, Sabi alisema jitihada za benki hiyo katika kuendeleza sekta ya michezo nchini kwa kiasi kikubwa inachagizwa na imani ya benki hiyo kuwa sanaa na michezo ni nguzo ya ajira na kuunganisha taifa.

“Kwa mfano kupitia udhamini wetu kwenye ligi tatu muhimu za mpira wa miguu hapa nchini, mbali na kuzalisha vipaji tumezalisha ajira za moja kwa moja zaidi ya 7,000 na mamilioni ya ajira zingine kwenye mnyororo wa uchumi. Zaidi pia kupitia mbio hizi za NBC Dodoma Marathon kwa kushirikiana na wadau wetu mbalimbali tunalenga kukusanya fedha kusaidia juhudi za Serikali katika kuboresha ya afya ya mama na mtoto kupitia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na kutoa ufadhili kwa wakunga,’’ alisema.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Damas Ndumbaro (kushoto) akipokea sweta maalum la mbio za NBC Dodoma Marathon kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi ikiwa ni ishara ya kumkaribisha rasmi Waziri huyo kwenye mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Julai 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma zikiwa na lengo la  kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na  kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga  ili kuboresha afya ya mama wa mtoto Makabiziano hayo yamefanyika  makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam leo.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kulia) akimpongeza Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Damas Ndumbaro (kushoto) baada ya kuthibitisha dahamira yake ya kukimbia km 42 kwenye mbio za NBC Dodoma Marathon zinazoratibiwa na benki hiyo kwa lengo la  kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na  kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga  ili kuboresha afya ya mama wa mtoto. Dkt Ndumbaro  amethibitisha dhamira hiyo leo jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Damas Ndumbaro (kushoto) akimpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio za NBC Dodoma Marathon Bi Tatiana Masimba kwa maandalizi mazuri yam bio hizo zinazotarajiwa kufanyika Julai 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma zikiwa na lengo la  kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na  kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga  ili kuboresha afya ya mama wa mtoto


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Damas Ndumbaro (kushoto) akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu mbio za NBC Dodoma Marathon pamoja mchango wa benki ya NBC katika kuendeleza sekta ya michezo nchini.   Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi



Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kulia) akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu mbio za NBC Dodoma Marathon pamoja mchango wa benki ya NBC katika kuendeleza sekta ya michezo nchini. Kushoto ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Damas Ndumbaro.

SASA RIADHA NA WAANDAAJI " RACE ORGANIZERS" DAM DAM

March 05, 2023

 

Kutoka Kulia: Ofisa wa BMT Charles Maguzu, Makamu wa Rais William Kallaghe na Mjumbe wa Kanda ya Kaskazini Alfredo Shahanga.


NA TULLO CHAMBO, RT

BAADA ya kutokea sintofahamu ya muda mrefu kati ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), na waandaaji wa matukio mbalimbali ya mbio za barabarani (RO's), hatimaye imefikia tamati.

Tamati hiyo imefikiwa baada ya kikao cha pamoja kati ya RT, RO's na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Machi 4 mwaka huu.
Katika kikao hicho kilichokuwa chini ya Makamu wa Rais wa RT , William Kallaghe na Ofisa Michezo BMT, Charles Maguzu, kilijadili kwa kina changamoto zinazokabili pande zote tatu.
Baada ya majadiliano ya takribani saa sitaa, pande zote zilipitia vifungu mbalimbali vya kikanuni na kuafikiana kuziheshimu ili kujenga ustawi bora wa mchezo wa riadha nchini.

Kikubwa kilichokaziwa, ni waandaaji kuheshimu mamlaka zilizopo na mamlaka kutenda haki kwa wateja wao (RO's).
Kikubwa Makamu wa Rais wa RT, Kallaghe aliwataka waandaaji kuheshimu na kushirikiana vyema na vyama vya riadha vya mikoa, na kwamba kuanzia hivi sasa waandaaji wanatakiwa kupata baraka za vyama vya mikoa kabla ya kuanza kutangaza matukio yao.

RT YATEKELEZA MAAGIZO YA BMT

March 05, 2023

 

Kulia ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania RT , Ndugu William Kallaghe akikabidhi ripoti kwa Katibu Mkuu Mtendaji wa BMT, Bi. Neema Msitha Jijini Dar es Salaam.


SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), Machi 3, 2022, limetekeleza agizo la Baraza la Michezo la Taifa (BMT), baada ya kukabidhi ripoti ya mapato na matumizi.

Ripoti hiyo imekabidhiwa na Makamu wa Rais wa RT, William Kallaghe, kwa Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha.
BMT ilifanya kikao na Kamati ya Utendaji ya RT,    Januari 21 kwenye moja ya kumbi za Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, na moja ya maelekezo ya Baraza, ilikuwa ni kuitaka RT kuwasilisha ripoti ya mapato na matumizi 2020/21 hadi 2021/22.

Baada ya kuipokea ripoti hiyo, Katibu Mtendaji BMT, Msitha, alisema watakaa na kuifanyia kazi.

RT YAWATAKA WATAALAM WA RIADHA NCHINI KUWASILISHA TAARIFA ZAO

February 05, 2023

 





NA TULLO CHAMBO, RT

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limewataka wataalamu wote wa mchezo huo kuwasilisha taarifa zinazoonyesha fani zao.
Agizo hilo, limetolewa na Kaimu Katibu Mkuu RT, Wakili Jackson Ndaweka, ambako amewataka makatibu wa vyama vya riadha mikoa yote ya Tanzania Bara, kuwajulisha wataalam wa riadha waliopo mikoani mwao, kuwasilisha taarifa zinazoonyesha fani zao katika mchezo huo. 

Wakili Ndaweka,amesema RT inakusudia kuendesha kozi mbalimbali za kuboresha uwezo wa wataalamu wa mchezo wa riadha waliopo na kuzalisha wengine katika fani ambazo zina upungufu. 

"Ili mpango huu uweze kutekelezeka kwa ufanisi, ni lazima kuwa na taarifa za wataalamu wa Riadha nchini, zitakazowezesha kuainisha maeneo yenye upungufu na kuyawekea mpango maalum," alisema na kufafanua. 

Taarifa zinazotakiwa zinapaswa kuwasilishwa kupitia wasifu 'CV', ambayo inapaswa kuambatanishwa na vivuli vya vyeti vya elimu ya Riadha na elimu ya kawaida. 

Wakili Ndaweka, alisema takwimu hizo ni muhimu sana kwa maendeleo ya mchezo wa riadha nchini. 

"Makatibu wanapaswa kuwajulisha wataalam waliopo kwenye mikoa yao, wawasilishe taarifa hizo kupitia anuani ya barua pepe ya shirikisho ambayo ni tan@mf.worldathletics.org si zaidi ya tarehe 20/02/2023," alisisitiza Ndaweka.

RT YAANIKA MATUKIO MANNE MAKUBWA YA KIMATAIFA 2023

February 04, 2023

 


| Yataka ushirikiano, uwajibikaji ngazi zote

|Timu ya Cross Country kuagwa Februari 14

NA TULLO CHAMBO, RT

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limeanika matukio manne makubwa ya kimataifa yanayolikabili mwaka 2023 na kusisitiza uwajibikaji wa pamoja kwa ngazi zote ili kuleta matokeo chanya.

Akizungumza na Wanahabari jijini Mwanza Februari 3, Rais wa RT, Silas Lucas Isangi, ameyataja matukio hayo ni Mashindano ya Mbio za Nyika 'Cross Country' ya Dunia, Bathurst, Australia Februari 18, Mashindano ya Vijana Afrika Mashariki (EAAR), U 18 na 20 Tanzania itakuwa mwenyeji Machi 10-11.

Tukio la tatu, Isangi alitaja ni Mashindano ya Afrika U 18 na 20 Lusaka Zambia  Aprili 27 hadi Mei 3.

"Pia kuna mashindano ya Common Wealth U 18 huko Trinidad na Tobago Agosti 4-11, vile vile All Africa Games Julai 4-23 nchini Ghana na Mashindano ya Dunia Budapest, Hungary" alisema na kuongeza.

Kwa kifupi mwaka huu uko bize sana, hivyo viongozi wa Riadha ngazi za chini kabisa, lazima wote tuamke na kutimiza wajibu kwa vitendo.

Rais Isangi, aliitaka mikoa yote ifanye mashindano ya vijana ili kufanikisha upatikanaji wa timu ya Taifa U 18 na 20 yenye tija. Pia ushiriki wao kwenye mashindano ya Taifa uwe wenye tija.

TIMU YA TAIFA CROSS COUNTRY
Rais Isangi, amesema timu hiyo imeanza kambi toka Februari Mosi katika Hoteli ya Mvono, Ngaramtoni jijini Arusha kwa gharama za shirikisho asilimia 100.

Amesema, timu itakaa kambini hadi Februari 12, itakapokwenda jijini Dar es Salaam tayari kwa kuagwa Februari 14, kabla ya kukwea pipa kwa safari ya Australia.

Amesema timu hiyo itakuwa chini ya Kiongozi wa msafara, Wakili Jackson Ndaweka ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu RT, Kocha Denis Male, huku wachezaji ni Mathayo Sombi, Inyasi Sulle, Fabian Nelson na Josephat Gisemo.

"Maandalizi yote yamekamilika ikiwamo tiketi, visa na vibali vyote vya serikali vimekamilika," alisema na kuishukuru serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kwa kusaidia katika maandalizi hayo.

MIKOA YATAKIWA KUHAKIKISHA MASHINDANO YA RIADHA VIJANA YANAANZIA NGAZI YA WILAYA

January 27, 2023

 


Kaimu Katibu Mkuu RT, Wakili Jackson Ndaweka.

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limeitaka mikoa yote nchini kuhakikisha inaendesha mashindani ya Vijana chini miaka 20 na 18 'U-20 U-18' kuanzia ngazi ya Wilaya.


Maelekezo hayo yametolewa na Kaimu Katibu Mkuu RT, Wakili Msomi Jackson Ndaweka, katika barua yake ya Januari 25 kwenda kwa viongozi wa vyama vya mikoa Tanzania Bara.


Amewaelekeza viongozi hao, kukumbuka kwamba kuna jukumu kubwa mbele yao, kwani mwaka huu una mashindano mengi ya vijana wa umri huo.


 Wakili Ndaweka, aliyataja mashindano hayo kuwa ni Afrika Mashariki U-18 na 20, Tanzania ikiwa mwenyeji, ambapo awali yalikuwa yamepangwa kufanyika Kigali, Rwanda.


Alisema, mashindano hayo yatafuatiwa na ya Afrika kwa umri huo Lusaka, Zambia Aprili 27 hadi Mei 3, 2023.


"Ili kuhakikisha nchi inashiriki kwa mafanikio mashindano hayo, lazima mashindano yaanzie ngazi ya Wilaya, kisha Mkoa na mwisho mashindano ya Taifa ya Wazi kwa vijana wa umri huo ambayo yanatarajiwa kufanyika Februari 25," alisema na kuongeza.


 Mashindano ya Wilaya yafanyike kati ya Februari 9-11 na Mikoa Februari 13-19.

 

"Utaratibu huu, unakusudia kuhakikisha wanapatikana wachezaji wenye uwezo mkubwa, ili kuleta tija katika ushiriki wa nchi kwenye mashindano ya kimataifa," alisema Wakili Ndaweka. 


Sambamba na hilo, RT inakusudia na imejipanga kuhakikisha kuwa kalenda yake inafuatwa na matukio yote yanafanyika kama yalivyopangwa.

 

Copyright © 2015 - 2025 Athletics Tanzania All Right Reserved

Developed by Gadiola Emanuel
Theme By AP | Developed By Gadiola Emanuel