Showing posts with label News. Show all posts
Showing posts with label News. Show all posts

MAPOKEZI YA RAIS WA RT ROGATH JOHN STEPHEN AKHWARI JIJINI ARUSHA

August 18, 2025

 

Kocha Mwingereza akimpongeza rais wa shirkisho la Riadha Tanzania -RT Kocha Rogath John Stephen Akhwari wakati wa mapokezi katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha Leo.

Mke wa Rogath John (katikati mwenye jaketi jekundu) akimpongeza mume wake kwa kuchaguliwa kuwa rais wa shirikisho la Riadha Tanzania -RT wakati wa mapokezi katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha Leo.
Rais wa shirikisho la Riadha Tanzania -RT Kocha Rogath John Stephen Akhwari Akiwashukuru Watanzania wote kwa Kumuombea na hatimaye kuchaguliwa kuwa rais , pia amechukua nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake kwenye michezo.


Na John Mhala, Arusha.

ARUSHA: Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) Rogath John Stephen Akhwari amesema safari ya kuendeleza mchezo wa riadha ndio imeanza kwani shirikisho hilo litaanzisha rasmi mbio za watoto na vijana lengo ni kuwatayarisha wenye umri huo kuwa kurithi mikoba ya wanariadha wanaojiandaa kustaafu.

Stephen amesema hayo leo alfajiri alipowasili jijini Arusha akitokea Mwanza baada ya kuchaguliwa na wajumbe wa RT kuwa Rais wa Shirikisho hilo na kusema kuwa wakati umefika sasa wa kuwaandaa watoto na vijana kushiriki mchezo wa riadha ili waweze kushika nafasi za akina Alphonce Simbu ,Magdalena Shauri,Jackline Sakilu na Gabriel Geay watakapostaafu.

Amesema RT lazima ijiandae kwa kuwaanda watoto na vijana ili waupende mchezo huo na hatimaye waweze kufanya vizuri kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na kushika zile nafasi walizofanya vizuri wanariadha wenzao hivyo wale wote wanaoanzisha na walioanzisha mbio kote nchini kipaumbele ni kuanzisha mbio za watoto na vijana mara moja kwani ndio lengo la msingi la kukuza mchezo huo unapendwa kwa sasa hapa nchini.

Rais huyo amesema ajira kwa sasa ni ngumu iwe ndani ya serikali na nje ya serikali na ajira nzuri ni mchezo wa riadha hivyo aliwaasa wazazi kuwapa ushirikiano watoto na vijana kujikita katika mchezo huo kwani una pesa nyingi kwa muda mfupi na kutoa mfano Simbu aliposhinda mbio za Boston amepata fedha nyingi ambazo hata waziri akistaafu serikali hawezi kuzipata.

Rogath ambaye mwajiriwa wa jeshi la Polisi nchini na kituo chake cha kazi Polisi Kati Arusha kwa cheo cha Mrakibu Msaidizi Mwandamizi (ASP) alimshukuru sana Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Inspekta General wa Polisi, Camilius Wambura kwa kumpa baraka za kuchukua fomu za kuwania kinyang’anyanyiro hicho na hatimaye kushinda urais.

CRDB BANK MARATHON YAFANYIKA DAR

August 17, 2025


Dar es Salaam, 17 Agosti 2025 - Maelfu ya wakimbiaji na wapenda michezo kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejitokeza leo katika viwanja vya The Green, Oysterbay, kushiriki CRDB Bank Marathon 2025, mbio za hisani ambazo mwaka huu zimekusanya Shilingi Bilioni 2 ili kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo, wakinamama wenye ujauzito hatarishi, na vijana kupitia programu ya iMBEJU.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, aliongoza maelfu ya washiriki kwenye msimu huu wa sita wa CRDB Bank Marathon. 
Akitoa salamu zake, Dkt. Tulia alipongeza ubunifu wa CRDB Bank Foundation katika kuunganisha jamii kupitia michezo na kusaidia wenye uhitaji, akieleza kuwa mbio hizo ni mfano wa vitendo vya huruma vinavyogusa maisha ya wengi. 
 
“Ushiriki wetu katika CRDB Bank Marathon ni tendo la huruma linaloleta faraja kwa watoto na wakinamama na familia zao. Ni ushahidi kwamba tukishirikiana, tunaweza kubadilisha maisha,” alisema.
Akitoa salamu zake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, aliipongeza Benki ya CRDB na CRDB Bank Foundation kuendelea kuandaa mbio hizo. 
 
Alisema, “CRDB Bank Marathon si tu imekuwa ikikuza afya na mshikamano wa kijamii, bali pia imekuwa ikifungua milango ya ajira na fursa za kiuchumi kwa vijana wetu. Michezo ni sekta inayoweza kubadili maisha, na ninapongeza sana kitendo cha kuweka zawadi nono kwa washindi. Hizi ni fursa ambazo zinaweza kuwa mtaji wa kuanzisha biashara na kuimarisha maisha ya vijana wetu. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kama CRDB Bank Foundation kuhakikisha michezo inakuwa chachu ya maendeleo ya taifa.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alibainisha kuwa msimu wa sita wa CRDB Bank Marathon umefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Benki ya CRDB, na kuendelea kupanua wigo wa matokeo yake ndani na nje ya Tanzania. Kwa mara ya pili, mbio hizi zimefanyika pia nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), zikikusanya fedha kwa ajili ya miradi ya afya na ustawi wa jamii katika nchi hizo. 

Nsekela alisema kuwa mbio za mwaka huu zimeweza kuvutia zaidi ya washiriki 16,000, na kufanikisha lengo la kukusanya shilingi bilioni 2 ambapo pamoja na kusaidia maandalizi ya mbio hizo, shilingi milioni 450, zimeelekezwa kusaidia wenye uhitaji katika jamii. 
 
Kati ya hizo shilingi milioni 100 zimekwenda hospitali ya CCBRT kusaidia wakinama wenye ujauzito hatarishi kujifungua salama, shilingi milioni 100 zimekwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kusaidia upasuaji wa Watoto wenye matatizo ya moyo, na shilingi 250 zitaelekezwa katika uwezeshaji wa vijana.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya mbio hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, alieleza kuwa safari ya msimu wa sita imeanzia Lubumbashi, DRC, ambako zilikusanywa Dola za Marekani 70,000 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali ya Jeshi la Ruashi, na kuendelea Bujumbura, Burundi, ambapo zilipatikana Faranga za Burundi milioni 175 kusaidia bima ya afya kwa zaidi ya watu 58,000 wasiojiweza. 
 
Mwambapa alisisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya mshikamano wa kipekee wa serikali za nchi shiriki, wadhamini na washiriki, akiwashukuru wadau wote waliotoa jitokeza kuchangia ikiwamo kampuni za bima za Sanlam Life na Alliance Life ambao wamekuwa sehemu ya mbio hizi tangu kuanzishwa kwake.
Washindi wa mbio za mwaka huu upande wa Tanzania kwa Kilometa 42 upande wa wanawake ni Joyloyce Kemuma kutoka Kenya, upande wa wanaume mshindi ni Abraham Kiptum kutoka Kenya. Kilometa 21 upande wa wanawake ni Catherine Syokau kutoka Kenya, na upande wa wanaume ni Joseph Panga kutoka Tanzania. Kilometa 10 upande wa wanawake ni Silia Ginoka kutoka Tanzania, na upande wa wanaume ni Boayi Maganga kutoka Tanzania.
 
Joseph Panga mshindi wa mbio za Kilometa 21 upande wa wanawake ameeleza furaha yake kushiriki katika mbio hizo na kusema kuwa ushindi wake ni sehemu ya kusaida matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo na matibabu ya wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT. 
 
“Mimi kama Mtanzania najisikia fahari kubwa kushiriki kusambaza tabasamu kwa watoto na wakinamama. Ni muhimu watu kufahamu kuwa afya bora ni haki ya kila mtoto, na hakuna mama anayestahili kupoteza maisha wakati wa kujifungua. Tunawashukuru CRDB Bank Foundation kwa kutuleta pamoja katika harakati hizi za kuokoa maisha,” amesema.
CRDB Bank Marathon imekuwa jukwaa muhimu la kuchochea ustawi wa kijamii katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na kati hivi karibuni ikipata heshima ya kutambuliwa kimataifa kwa kushinda tuzo ya jukwaa bora la taasisi za fedha katika kusaidia kusaidia jamii.

ROGATH JOHN STEPHEN AKHWARI ACHAGULIWA KUWA RAIS WA SHIRIKISHO LA RIADHA TANZANIA

August 17, 2025

 

Kocha wa Polisi Tanzania na Katibu Mkuu wa Riadha Chama cha Mkoa wa Arusha Rogath John Stephen Akhwari amechaguliwa na wajumbe kuwa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania huko Mwanza tarehe 16/08/2025 kwa kupata Kura 27 kati ya 47 na mpinzani wake Bw. Nsolo Malongo Mlozi kupata kura 20. 
Wakili Jackson Beda Ndaweka Achaguliwa kuwa Makamu wa Shirikisho la Riadha Tanzania -RT , baada ya kuitumikia shirikisho la riadha Tanzania kama Kaimu Katibu Mkuu kwa Muda mrefu.

GEAY 'AKICHAFUA' MBEYA TULIA MARATHON 2023

May 06, 2023


 

BINGWA wa Taifa anayeshikilia rekodi ya Marathon Tanzania, Gabriel Gerald Geay amekuwa kivutio kikubwa Mbeya Tulia Marathon, aliposhiriki na kuibuka mshindi katika mbio za mita 1500.

Mbeya Tulia Marathon, imekata utepe Leo Mei 5 kwa mbio za uwanjani, kabla ya kesho Jumamosi Mei 6 kurindima Marathon.

Katika mbio hizo za mita 1500, Geay alianza taratibu raundi ya kwanza akiwa nyuma, kabla ya mzunguko wa pili kupata dhoruba la kuangushwa, lakini alinyanyuka na kukiwasha na hatimaye kuibuka mshindi akitumia dakika 3:58.46.

Geay alifuatiwa na Faraja Damas wa JWTZ aliyetumia dakika 4:00.08 huku nafasi ya tatu ikienda kwa John Joseph pia JWTZ 4:06.25. 

Mashabiki na viongozi mbalimbali waliojitokeza, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa, walishindwa kujizua kumshangilia Geay wakati akikiwasha katika mbio hizo.

Kwa upande wa wanawake Mita 1500, Magdalena Shauri wa JWTZ, alishinda akitumia dakika 4:31.13 na kufuatiwa na Salma Charles ambaye katoka Zambia na Timu ya Taifa U 18 na 20 iliyoshiriki mashindano ya Afrika, dakika 4:46.55 na wa tatu akiwa ni Mayselina Mbua JWTZ 4:53.16.

Mbali na Geay ambaye katoka kufanya kweli katika mbio kongwe za Boston Marathon nchini Marekani alikoshika nafasi ya pili hivi karibuni, pia mkali mwingine, ambaye pia ni Mshindi wa medali ya Fedha Jumuiya na Mwanamichezo Bora Tuzo za BMT 2022, Alphonce Simbu, naye alikuwepo kushuhudia mbio hizo.

Pia, Timu ya Taifa ya Vijana iliyopumzika hapa ikitokea Ndola Zambia ilikojinyakulia medali mbili katika mashindano ya Afrika, baadhi walipata nafasi ya kushiriki mbio za uwanjani Mbeya Tulia Marathon.

Timu hiyo inatarajiwa kuondoka Mbeya kesho Jumapili kurejea Dar es Salaam.

Pia, mbio hizo zilipambwa program ya watoto 'Kids Athletics', ambayo ilikuwa kivutio kwa watoto wa shule za msingi walioshiriki.

JK AKUTANA NA MWANARIADHA WA KIMATAIFA GABRIEL GERALD GEAY BOSTON, MAREKANI

April 19, 2023

 Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na wanariadha Gabriel Geay (kushoto kwake) na Wence Tarimo (kulia kwake) ambao walishiriki katika Mashindano ya Riadha yaliyofanyika Boston, Marekani tarehe 17 Aprili 2023, ambapo Geay aliibuka mshindi wa pili. Kulia ni Mhe. Saada Mkuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Fedha na Uchumi - wa Zanzibar.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akipokea zawadi ya jezi toka kwa mhamasishaji mashuhuri Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo wakati alipoonana na wanariadha Gabriel Geay (kushoto kwake) na Wence Tarimo (kulia kwake) ambao walishiriki katika Mashindano ya Riadha yaliyofanyika Boston, Marekani tarehe 17 Aprili 2023, ambapo Geay aliibuka mshindi wa pili. Kulia ni Mhe. Saada Mkuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Fedha na Uchumi - wa Zanzibar.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini kwenye kitabu cha mwanariadha Gabriel Geay mjini Boston Marekani, siku moja baada ya shujaa huyo kushika nafasi ya pili kwenye mbio za Boston Marathon.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na wanariadha Gabriel Geay (kushoto kwake) na Wence Tarimo (kulia kwake) ambao walishiriki katika Mashindano ya Riadha yaliyofanyika Boston, Marekani tarehe 17 Aprili 2023, ambapo Geay aliibuka mshindi wa pili. Kulia ni Mhe. Saada Mkuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Fedha na Uchumi - wa Zanzibar na kushoto ni mhamasishaji mashuhuri Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mhe. Saada Mkuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Fedha na Uchumi - wa Zanzibar wakiwa na Watanzania waishio Marekani pamoja na wanariadha Gabriel Geay na Wence Tarimo ambao walishiriki katika Mashindano ya Riadha yaliyofanyika Boston, Marekani tarehe 17 Aprili 2023, ambapo Geay aliibuka mshindi wa pili. Kulia ni mhamasishaji mashuhuri Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo na kushoto ni mtoto wa Bongo Zozo.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi kitabu mwanariadha Gabriel Geay mjini Boston Marekani, siku moja baada ya shujaa huyo kushika nafasi ya pili kwenye mbio za Boston Marathon.

*******

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekutana na Wanariadha Gabriel Geay na Wence Tarimo walioshiriki katika Mashindano ya Marathon yaliyofanyika Boston, Marekani tarehe 17 Aprili 2023.

Gabriel Geay aliibuka mshindi wa pili katika mashindano hayo. Mheshimiwa Rais Mstaafu amempongeza Gabriel Geay kwa ushindi mkubwa na kwa kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Pamoja na wanariadha hao, walikuwepo pia wahamasishaji mbalimbali akiwemo “Bongo Zozo”. Amewapongeza pia kwa kuhamasisha ushindi huu na kufanikisha kuinua bendera ya Tanzania juu.

Mheshimiwa Rais Mstaafu yuko Boston, Marekani ambapo anashiriki katika kutoa mafunzo kwa Mawaziri wa Fedha kutoka nchi mbalimbali zinazoendelea kupitia Mpango wa Uongozi wa Harvard “Harvard Ministerial Leadership Program”.

Katika mafunzo hayo, Mhe. Saada Mkuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Fedha na Uchumi - wa Zanzibar ameshiriki pia.

RT YAUONGEZEA THAMANI UWANJA WA BENJAMIN MKAPA, DAR

March 12, 2023

 







 NA TULLO CHAMBO, RT


SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), kwa ushirikiano na shirikisho la mchezo huo nchini Kenya (AK), wamezindua kifaa maalum cha kupima hali ya hewa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kifaa hicho ni maalumu kwa ajili ya kupima ubora wa hali ya hewa sehemu husika, kama iko sawa kwa matumizi ya wanamichezo shiriki wakati wa tukio ama haiko sawa.

Ufungaji wa kifaa hicho ni maagizo ya Shirikisho la Riadha la Kimataifa (WA), ambapo Tanzania imekuwa nchi ya nne barani Afrika kupata teknolojia hiyo. 

Akizungumza  wakati wa uzinduzi huo mbele ya Mgeni rasmi Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, Rais wa AK ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Riadha Ukanda wa Afrika Mashariki (EAAR), Luteni Jenerali mstaafu Jackson Tuwei, alisema kifaa hicho ni muhimu kwani binadamu hata wanyama wanahitaji kuishi katika mazingira ya hali ya hewa safi.

Luteni Jenelari Tuwei, alisema teknolojia hiyo imeanza kutumika nchini Kenya, kisha ilifuatiwa na Dakar Senegal, Addis Ababa Ethiopia na Tanzania imekuwa ni nchi ya nne kufungwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na badae wanatarajia kufunga kifaa hicho nchini Zambia ambako yanatarajiwa kufanyika mashindano ya vijana Afrika Aprili 27 hadi Mei 3.

Kwa upande wake, Katibu wa BMT, Neema Msitha, alishukuru kwa jambo hilo ambalo linauongezea thamani wa Uwanja wa Benjamin Mkapa kimataifa, na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, mbali ya kuipongeza RT kwa kufanikisha jambo hilo lenye manufaa kwa wanamichezo wote watakaokuwa wanautumia uwanja huo, iko tayari kutoa Ushirikiano katika kila  jambo lenye maendeleo kwenye sekta ya michezo na kwamba wadau wote wa michezo wanakaribishwa.

Kifaa hicho kimetengenezwa na taasisi ya mazingira nchini Sweden ijulikanayo kama Stocklohom Environment Instute (SEI).

SASA RIADHA NA WAANDAAJI " RACE ORGANIZERS" DAM DAM

March 05, 2023

 

Kutoka Kulia: Ofisa wa BMT Charles Maguzu, Makamu wa Rais William Kallaghe na Mjumbe wa Kanda ya Kaskazini Alfredo Shahanga.


NA TULLO CHAMBO, RT

BAADA ya kutokea sintofahamu ya muda mrefu kati ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), na waandaaji wa matukio mbalimbali ya mbio za barabarani (RO's), hatimaye imefikia tamati.

Tamati hiyo imefikiwa baada ya kikao cha pamoja kati ya RT, RO's na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Machi 4 mwaka huu.
Katika kikao hicho kilichokuwa chini ya Makamu wa Rais wa RT , William Kallaghe na Ofisa Michezo BMT, Charles Maguzu, kilijadili kwa kina changamoto zinazokabili pande zote tatu.
Baada ya majadiliano ya takribani saa sitaa, pande zote zilipitia vifungu mbalimbali vya kikanuni na kuafikiana kuziheshimu ili kujenga ustawi bora wa mchezo wa riadha nchini.

Kikubwa kilichokaziwa, ni waandaaji kuheshimu mamlaka zilizopo na mamlaka kutenda haki kwa wateja wao (RO's).
Kikubwa Makamu wa Rais wa RT, Kallaghe aliwataka waandaaji kuheshimu na kushirikiana vyema na vyama vya riadha vya mikoa, na kwamba kuanzia hivi sasa waandaaji wanatakiwa kupata baraka za vyama vya mikoa kabla ya kuanza kutangaza matukio yao.

 

Copyright © 2015 - 2025 Athletics Tanzania All Right Reserved

Developed by Gadiola Emanuel
Theme By AP | Developed By Gadiola Emanuel