
Wanariadha 8 wakiwemo wa Mbio za Uwanjani, Mbio ndefu na Mrusha mkuki, wameondoka kwenda Accra , Ghana kushiriki mashindano ya Afrika “All African Games” ambayo yalianza toka tarehe 8 Machi hadi 23 Machi 2024.
Copyright @gettyimages
Hongera kwa Andrew Boniface Rhobi kutoka jeshi la polisi Tanzania kwa kupata muda wako bora wa dakika tatu na sekunde hamsini na moja ( 3:51.44) yaani ( Personal Best) mita 1500 (1500M) na kuwa nafasi ya Saba kwenye heat ya kwanza, kwenye Mashindano ya Dunia ya Ndani ( World Athletics indoors Championships Glasgow 2024) tarehe 1-3 Machi 2024, huko Glasgow, Scotland.
BINGWA wa Taifa anayeshikilia rekodi ya Marathon Tanzania, Gabriel Gerald Geay amekuwa kivutio kikubwa Mbeya Tulia Marathon, aliposhiriki na kuibuka mshindi katika mbio za mita 1500.
Mbeya Tulia Marathon, imekata utepe Leo Mei 5 kwa mbio za uwanjani, kabla ya kesho Jumamosi Mei 6 kurindima Marathon.
Katika mbio hizo za mita 1500, Geay alianza taratibu raundi ya kwanza akiwa nyuma, kabla ya mzunguko wa pili kupata dhoruba la kuangushwa, lakini alinyanyuka na kukiwasha na hatimaye kuibuka mshindi akitumia dakika 3:58.46.
Geay alifuatiwa na Faraja Damas wa JWTZ aliyetumia dakika 4:00.08 huku nafasi ya tatu ikienda kwa John Joseph pia JWTZ 4:06.25.
Mashabiki na viongozi mbalimbali waliojitokeza, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa, walishindwa kujizua kumshangilia Geay wakati akikiwasha katika mbio hizo.
Kwa upande wa wanawake Mita 1500, Magdalena Shauri wa JWTZ, alishinda akitumia dakika 4:31.13 na kufuatiwa na Salma Charles ambaye katoka Zambia na Timu ya Taifa U 18 na 20 iliyoshiriki mashindano ya Afrika, dakika 4:46.55 na wa tatu akiwa ni Mayselina Mbua JWTZ 4:53.16.
Mbali na Geay ambaye katoka kufanya kweli katika mbio kongwe za Boston Marathon nchini Marekani alikoshika nafasi ya pili hivi karibuni, pia mkali mwingine, ambaye pia ni Mshindi wa medali ya Fedha Jumuiya na Mwanamichezo Bora Tuzo za BMT 2022, Alphonce Simbu, naye alikuwepo kushuhudia mbio hizo.
Pia, Timu ya Taifa ya Vijana iliyopumzika hapa ikitokea Ndola Zambia ilikojinyakulia medali mbili katika mashindano ya Afrika, baadhi walipata nafasi ya kushiriki mbio za uwanjani Mbeya Tulia Marathon.
Timu hiyo inatarajiwa kuondoka Mbeya kesho Jumapili kurejea Dar es Salaam.
Pia, mbio hizo zilipambwa program ya watoto 'Kids Athletics', ambayo ilikuwa kivutio kwa watoto wa shule za msingi walioshiriki.
NA TULLO CHAMBO, RT
SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), kwa ushirikiano na shirikisho la mchezo huo nchini Kenya (AK), wamezindua kifaa maalum cha kupima hali ya hewa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Kifaa hicho ni maalumu kwa ajili ya kupima ubora wa hali ya hewa sehemu husika, kama iko sawa kwa matumizi ya wanamichezo shiriki wakati wa tukio ama haiko sawa.
Ufungaji wa kifaa hicho ni maagizo ya Shirikisho la Riadha la Kimataifa (WA), ambapo Tanzania imekuwa nchi ya nne barani Afrika kupata teknolojia hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo mbele ya Mgeni rasmi Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, Rais wa AK ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Riadha Ukanda wa Afrika Mashariki (EAAR), Luteni Jenerali mstaafu Jackson Tuwei, alisema kifaa hicho ni muhimu kwani binadamu hata wanyama wanahitaji kuishi katika mazingira ya hali ya hewa safi.
Luteni Jenelari Tuwei, alisema teknolojia hiyo imeanza kutumika nchini Kenya, kisha ilifuatiwa na Dakar Senegal, Addis Ababa Ethiopia na Tanzania imekuwa ni nchi ya nne kufungwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na badae wanatarajia kufunga kifaa hicho nchini Zambia ambako yanatarajiwa kufanyika mashindano ya vijana Afrika Aprili 27 hadi Mei 3.
Kwa upande wake, Katibu wa BMT, Neema Msitha, alishukuru kwa jambo hilo ambalo linauongezea thamani wa Uwanja wa Benjamin Mkapa kimataifa, na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, mbali ya kuipongeza RT kwa kufanikisha jambo hilo lenye manufaa kwa wanamichezo wote watakaokuwa wanautumia uwanja huo, iko tayari kutoa Ushirikiano katika kila jambo lenye maendeleo kwenye sekta ya michezo na kwamba wadau wote wa michezo wanakaribishwa.
Kifaa hicho kimetengenezwa na taasisi ya mazingira nchini Sweden ijulikanayo kama Stocklohom Environment Instute (SEI).
Kutoka Kulia: Ofisa wa BMT Charles Maguzu, Makamu wa Rais William Kallaghe na Mjumbe wa Kanda ya Kaskazini Alfredo Shahanga.
![]() |
Wanariadha wakichuana kwenye mashindano ya Majaribio Jijini Dar es Salaam. |
Kulia ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania RT , Ndugu William Kallaghe akikabidhi ripoti kwa Katibu Mkuu Mtendaji wa BMT, Bi. Neema Msitha Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Katibu Mkuu RT, Wakili Jackson Ndaweka.
SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limeitaka mikoa yote nchini kuhakikisha inaendesha mashindani ya Vijana chini miaka 20 na 18 'U-20 U-18' kuanzia ngazi ya Wilaya.
Maelekezo hayo yametolewa na Kaimu Katibu Mkuu RT, Wakili Msomi Jackson Ndaweka, katika barua yake ya Januari 25 kwenda kwa viongozi wa vyama vya mikoa Tanzania Bara.
Amewaelekeza viongozi hao, kukumbuka kwamba kuna jukumu kubwa mbele yao, kwani mwaka huu una mashindano mengi ya vijana wa umri huo.
Wakili Ndaweka, aliyataja mashindano hayo kuwa ni Afrika Mashariki U-18 na 20, Tanzania ikiwa mwenyeji, ambapo awali yalikuwa yamepangwa kufanyika Kigali, Rwanda.
Alisema, mashindano hayo yatafuatiwa na ya Afrika kwa umri huo Lusaka, Zambia Aprili 27 hadi Mei 3, 2023.
"Ili kuhakikisha nchi inashiriki kwa mafanikio mashindano hayo, lazima mashindano yaanzie ngazi ya Wilaya, kisha Mkoa na mwisho mashindano ya Taifa ya Wazi kwa vijana wa umri huo ambayo yanatarajiwa kufanyika Februari 25," alisema na kuongeza.
Mashindano ya Wilaya yafanyike kati ya Februari 9-11 na Mikoa Februari 13-19.
"Utaratibu huu, unakusudia kuhakikisha wanapatikana wachezaji wenye uwezo mkubwa, ili kuleta tija katika ushiriki wa nchi kwenye mashindano ya kimataifa," alisema Wakili Ndaweka.
Sambamba na hilo, RT inakusudia na imejipanga kuhakikisha kuwa kalenda yake inafuatwa na matukio yote yanafanyika kama yalivyopangwa.
Sudan Kusini yaipa shavu RT, Simbu Balozi mpya JICA
NA TULLO CHAMBO, RT
MASHINDANO Maalum ya Riadha ya Wanawake nchini Tanzania maarufu kama Ladies First, yamezidi kufungua ushirikiano wa mchezo huo kimataifa.
Ladies First ikiwa ni wazo la Nguli wa Riadha nchini Tanzania, Kanali mstaafu Juma Ikangaa, imefanyika mwaka huu ukiwa ni msimu wa nne na kushirikisha mikoa 30 Kati ya 31 Tanzania Bara na Visiwani.
Mwaka huu, mashindano hayo yalifanyika January 21 na 22 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na kushirikisha zaidi ya wanariadha 186.
Kanali Mstaafu Ikangaa, ambaye enzi zake aliiwakilisha vema Tanzania kimataifa katika mbio za marathoni, ikiwemo nchini Japan, nchi hiyo imekuwa ikimuenzi na kumpa heshima kubwa ambapo hivi sasa ni Balozi wa Hiari wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA).
Katika kumuenzi Kanali Ikangaa, Japan ilimtaka kusema kitu ambacho nchi hiyo iifanyie Tanzania, ndipo kwa kushirikiana na wadau wake mbalimbali, akaja na wazo la kuwaenzi na kuhamasisha wanawake kushiriki katika mchezo wa Riadha, hasa ikizingatiwa medali ya kwanza ya kimataifa Tanzania ililetwa na Mwanamke Theresia Dismas mwaka 1964, katika michezo ya All Africa nchini Congo Brazzaville, kupitia mchezo wa Kurusha Mkuki 'Javelin'.
Wazo hilo lilianza kutekelezeka mwaka 2017 kwa mashindano yaliyofanyika Uwanja wa Taifa, sasa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ambapo baadhi ya washindi wamekuwa wakipata nafasi ya kwenda kushiriki mbio za Nagai City nchini Japan.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Tanzania (BMT), Bi. Neema Msitha, aliipongeza JICA na kampuni mbalimbali za Kijapan zinazofanya kazi nchini, Kanali Ikangaa,serikali ya Tanzania na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kwa kufanikisha mashindano hayo kwa msimu wa nne sasa.
Bi. Msitha, anasema mashindano hayo yalianza mwaka 2017 na kufanyika kwa mafanikio makubwa miaka mitatu mfululizo hadi 2019 kabla kusitishwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo janga la UVIKO 19 'Covid 19'.
"Lengo la mashindano haya ni kuhamasisha ushiriki wa watoto wa kike katika michezo hususan Riadha, kutoa fursa kwa wanariadha wa kike kuonyesha vipaji vyao na kuendeleza vipaji vya wanariadha ambao wataiwakilisha nchi katika mashindano ya kitaifa na kimataifa," anasema Bi. Msitha.
Tangu kuanza kwa mashindano hayo mwaka 2017, Wanariadha wa Tanzania na viongozi wao, wamekuwa wakipata nafasi ya kwenda kushiriki Nagai Marathon, ambapo wanariadha akiwemo Angel John Joseph Yumba, Fabian Nelson Sulle, Fabian Joseph, Alphonce Felix Simbu na wengineo wameweza kung'ara.
Mbali na hilo, Ladies First iliweza kuishirikisha nchi ya Sudan Kusini na kushiriki mashindano ya mwaka 2019 jijini Dar es Salaam.
Mwaka huu 2023, Ladies First imezidi kufungua milango katika mchezo wa Riadha Tanzania, ambapo Sudan Kusini iliwakilishwa na viongozi wake mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Michezo nchini humo, Peter Baptist, Balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania, Deng Abel na wengineo.
Baptist katika salamu zake, mbali na kushukuru na kupongeza Tanzania kwa mashindano hayo, anasema na kwao wana mashindano kama hayo yajulikanayo kama 'Umoja na Amani', yakilenga kutumia michezo kuhamasisha amani na umoja katika Taifa hilo ambalo liliandamwa na vita miongoni mwao kwa miaka kadhaa.
Mwakilishi huyo, anasema katika kuendeleza ushirikiano na Tanzania, wanatoa mwaliko kwa wanariadha wanne waliofanya vizuri katika Ladies First 2023 wa mbio tofauti ukiondoa mita 5000 kwenda Sudan Kusini kushiriki mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika miezi miwili ijayo.
Mbali na fursa hizo zilizojitokeza Ladies First 2023, nyingine ni kwa Mwanariadha anayefanya vema hivi sasa, Mshindi wa Medali ya Fedha Common Wealth Games 2022, Alphonce Simbu, naye kuteuliwa kuwa Balozi wa Hiari JICA, akiungana na Kanali mstaafu Ikangaa.
Haya ni kati ya mafanikio ya Ladies First 2023, na hakika uwajibikaji ukizidi kuongezeka, bila shaka milango zaidi itazidi kufunguka katika medani ya riadha Tanzania.
Copyright © 2015 - 2025 Athletics Tanzania All Right Reserved
Developed by Gadiola Emanuel