Matukio

< span data-type="recent" data-yes="5">

Gwajima Anogesha Ufunguzi wa LADIES FIRST Dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam

Waziri Dkt. Dorothy Gwajima wa pili kutoka Kulia, akishiriki Maoezi ya Viungo wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya Ladies First kwa msimu wa Nne, wa kwanza kutoka kulia ni Mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga, Balozi wa Japan Tanzania kushoto kwa Waziri, na Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Y. Msitha 


 NA TULLO CHAMBO - AT


MSIMU wa Nne wa Mashindano ya Riadha ya Wanawake maarufu kama 'Ladies First' umefunguliwa kwa kishindo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Januari 21 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy  Gwajima.

Mashindano hayo  ya siku mbili yameandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), kwa kushirikiana na  Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).
 
Ufunguzi huo, ulipambwa na vikundi mbalimbali vya Jogging, burudani mbalimbali akiwamo Msanii maarufu wa Singeli, Dullah Makabila, aliyepagawisha vilivyo na wanariadha wa kike.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Dkt. Gwajima, alisema wataendelea kuwekeza kwa watoto ngazi ya vijiji ili kuibua vipaji vipya, ambavyo vitapata fursa ya kushiriki mashindano mbalimbali kitaifa na kimataifa siku za mbeleni.

Pia, alisema watahakikisha wanasuka upya mikakati katika shule mbalimbali ili kupata muonekano mpya katika michezo.

"Nitoe wito kwa wazazi kutoa fursa kwa vijana wao wa kike, kujitokeza kushiriki michezo kwani ni ajira itakayosaidia kujikwamua kiuchumi katika familia zao," alisema Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, alisema lengo kubwa la mashindano hayo ni kuhamasisha watoto wa kike kushiriki katika michezo, kwani michezo ni fursa na ajira.

Aliwapongeza JICA kwa kufanikisha kwa kiasi kikubwa Mashindano hayo, RT, vyama vya Riadha vya Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa kwa kuwezesha wachezaji wao kufika Dar es Salaam kwa ajili ya mashindano hayo, Ofisi ya Mkurugenzi Manispaa ya Temeke kwa kuruhusu zaidi ya wanafunzi 1,000 kuhudhuria mashindano hayo na kujifunza, na Mwanariadha mahiri wa zamani, Kanali Mstaafu Juma Ikangaa, ambaye pia ni Balozi wa Hiari wa JICA, kwa kuasisi wazo la kuanzishwa mashindano hayo.

Balozi mwingine wa hiari wa JICA, Mwanariadha mshindi wa medali ya Fedha Jumuiya ya Madola, Alphonce Felix  Simbu, aliwataka wanariadha wa kike hao watumie fursa hiyo kujituma na kurejesha enzi za Mwanamama Theresia Dismas, ambaye ni mchezaji wa kwanza kuipa Tanzania medali ya kimataifa katika michuano ya All African Games 1965 Congo Brazaville.

Simbu, alisema kuwa ushiriki huo utakuwa chachu ya kujifikiria namna ya  Theresia Dismas alieweza kupata medali.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu RT, Wakili Jackson Ndaweka, aliishukuru Serikali kwa kuwezesha kupata muungano na JICA kwa kudhamini Riadha hususani kwa wanawake.
Àlisema kuwa wanawake wanatakiwa kutumia fursa ya kujiendeleza  ,kwani mahitaji kuleta ushindani . 

Mashindano hayo yatakayofikia tamati Januari 22, yanashirikisha wanariadha zaidi ya 186 kutoka mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.

Uzinduzi huo, pia ulihudhuriwa na Balozi wa Japan nchini Tanzania, viongozi kutoka Wizara ya Michezo Sudan Kusini, Naibu Meya Jiji la Nagai Japan, Mwenyekiti wa BMT Leodegar C. Tenga na Makamu wa Rais RT, William Kallaghe.

Post a Comment

0 Comments