Matukio

< span data-type="recent" data-yes="5">

Kumekucha Ladies First 2023, Wanawake Kuchuana DAR



NA TULLO CHAMBO


WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dr. Dorothy Gwajima, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mashindano Maalum ya Riadha ya Wanawake maarufu kama 'Ladies First' yanayotarajiwa kurindima kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa January 21 na 22 jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, alisema mashindano hayo yamendaliwa na BMT, Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), na kuwezeshwa na Shirika la Maendeleo la Japan ( JICA), na huu ni msimu wake wa nne,  yakiwa na lengo la kuwahamasisha wanawake kushiriki katika mchezo wa Riadha.


"Lengo la mashindano haya ni kuwahasisha  watoto wa kike kushiriki katika michezo hususan Riadha, kutoa fursa ya wanariadha wa like kuonyesha vipaji vyao na kuendeleza vipaji vya wanariadha ambao watawakilisha nchi katika mashindano ya kitaifa na kimataifa siku zijazo," alisema Msitha.


Alisema mashindano ya mwaka huu, yatashirikisha wanariadha 186 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani yakishirikisha mbio za Mira 100, 200, 400, 800, 1500, 5000, 10000, Kupokezana Vijiti 4x400 na Kurusha Mkuki na kushuhudiwa na watazamaji mbalimbali wakiwemo wanafunzi 1000 kutoka shule za Msingi na Sekondari za Manispaa ya Temeke.


"BMT inaishukuru Sana JICA na kampuni za Kijapan zinazofanya shughuli zake hapa nchini kwa kufadhili mashindano haya kwa mara ya  nne, pia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kutoa uwanja ambao utatumika kwa mshindano na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke ambayo imetoa ruhusa kwa wanafunzi kushiriki na kujifunza katika mashindano haya," alisema Msitha na kuongeza.


Baraza linaendelea kusisitiza Kamati za Michezo za Mikoa, kuhakikisha zunawezesha ushiriki wa wanaridha wa mikoa yao katika mashindano haya na kuwaomba wananchi wote wa Jiji la Dar es Salaam  kujitokeza kwa wingi siku ya Jumamosi na Jumapili kushuhudia mashindano hayo ambapo hakuna kiingilio.


Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania, Naofumi Yamura, alisema wanajivunia kuanza kutoa ushirikiano kwa Tanzania toka mwaka 1962 na mashindano ya mwaka huu watayatumia kama maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano wao na Tanzania.


Yamura, alisema mashindano ya mwaka huu yatahudhuriwa na watu mbalimbali maarufu akiwemo Balozi wa Japan Tanzania, viongozi kutoka Sudan ya Kusini, Mwanariadha nguli Kanali mstaafu Juma Ikangaa na mwanariadha anayewika hivi sasa Alphonce Simbu.


Naye Katibu wa Chama cha Riadha Zanzibar (ZAAA), Muhidin Masunzu akimwakilisha Kaimu Katibu Mkuu wa RT, Wakili Jackson Ndaweka, alisema wamejiandaa vema kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa ufanisi.


Wazo la kuanzishwa mashindano hayo liliasisiwa na Kanali Ikangaa, ambaye pia no Balozi wa Hiari wa JICA, likitokana na kuenzi historia ambapo medali ya kwanza Tanzania kimataifa ililetwa na Mwanamama Thereza Dismas, aliyekuwa akirusha Mkuki.

Post a Comment

0 Comments