Napenda
kuchukua nafasi hii kuushukuru uongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za
Michezo Tanzania (TASWA) kwa kuandaa hafla ya kutoa tuzo kwa wanamichezo 10
bora waliofanya vizuri kwa kuiletea heshima
nchi yetu katika miaka 10 ya uongozi wa mwanamichezo mwenzetu Mhe.
Jakaya Mrisho Kikwete,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pamoja
na kutoa tuzo kwa Wanamichezo bora waliofanya vizuri miaka 10 iliyopita, vile vile TASWA ilimtunuku tuzo Mhe Jakaya
Mrisho Kikwete kwa mchango wako katika michezo.
Mhe.
Rais, wakati anazungumza na wanamichezo waliokusanyika katika ukumbi wa Mlimani
hapo tarehe 12/10/2015 alisononeka kwa wanamichezo wa Tanzania kutofanya vizuri
wakati wa miaka 10 ya uongozi wake pamoja na kuleta walimu katika baadhi ya
vyama vya michezo.
Mafanikio
hata katika maisha ya kawaida ni mapambano hali kadhalika hata kupata mafanikio
katika michezo ni mapambano. Katika miaka ya 70-80 michezo ilikuwa ridhaa,
lakini kuanzia miaka ya 90 hadi sasa michezo imekuwa biashara na ajira kubwa
kwa wanamichezo.
Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa akimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuendeleza michezo katika kipindi chake chote cha uongozi wake wa miaka 10. |
Kwa
mfumo huo wa michezo kuwa biashara na ajira kila moja angefikiria kwamba
tungepaswa kuwa na wanamichezo wengi kwa
hiari yao kuchangamkia mazoezi ya hali ya juu ili nao waweze kuwa wawakilishi
wazuri wa nchi yetu na kujipatia zawadi nono za fedha, lakini badala yake hali
inazidi kuwa mbaya.
Hali
hii inawezekana vile vile imesababishwa na hali ya ukata wa vyama vya michezo
ambao hawana uwezo wa kutafuta vipaji huko walipo hasa Vijijini, Wilayani na
Mikoani.
Katika miaka ya 70-80, Vyama
vyetu vilikuwa vinapata ruzuku kutoka Serikalini kupitia Baraza la Michezo la
Taifa (BMT), ruzuku ambayo ilikuwa inawasaidia kuendesha ofisi na kuandaa
Mashindano kama ya Taifa ambayo
wanamichezo wengi wanakusanyika na vyama husika kufanya uteuzi wa wachezaji bora
wenye vipaji ambao huwaendeleza.
Huo mfumo kwa sasa haupo kutokana na hali
inayotamkwa na vyama vya michezo kama ukata na Serikali (BMT) kutokuwa na
fedha.
Katika risala yake wakati wa tuzo kwa
wanamichezo bora, Mhe. Rais alikiri bila kuwekeza tusitegemee kupata mafanikio,
lakini nani awekeze, kwa haraka kwa tulio na uelewa mdogo ni Serikali ndiyo
iwekeze kama nchi zingine duniani inavyofanya.
Mhe.
Rais amefanya mengi kuinua michezo wakati wa uongozi wake. Naomba nitaje
chache:
1. WALIMU WA MICHEZO KUTOKA NJE.
Aliweza
kuwalipa mishahara walimu wa michezo kama mpira wa miguu, netiboli, ngumi na
riadha (pamoja na walimu wa riadha kutokuwa wa viwango) kupitia mpango wa
ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba. Kila mmoja wetu aliona jitihada zake, na nakiri kwamba kwa namna moja au nyingine,
vyama/mashirikisho ya michezo hawakutekeleza wajibu wao kutokana na hali ya
ukata.
Hata wanamichezo wetu hawakutambua na kuona michezo kama ajira.
Mhe.
Rais anakiri mafanikio yana gharama, bila nchi kuwekeza hafikirii kama tutakuwa
na mwelekeo mwema hasa kwa vijana wetu kufanya vizuri katika medani ya
Kimataifa. Nchi nyingi zinazofanya vizuri katika michezo ya kimataifa kwa asilimia kubwa wamewekeza katika michezo.
Pamoja na WHVUM kutengewa bajeti ndogo ya michezo, bado suala la kuwekeza
haliwezi kukwepeka kwa hali ya sasa ya michezo duniani.
2. MICHEZO YA UMITASHUMTA/UMISSETA.
Tutakukumbuka
hasa pale Mhe Jakaya aliporejesha michezo ya Umitashumta na Umisseta mwaka 2007 baada ya kusimama kwa zaidi ya
miaka 9.
Binafsi
naamini kilichotufikisha hapa tulipo leo ni pamoja na kutofundishwa kwa elimu
ya viungo (PE) sambamba na kutokuwepo walimu wa masomo hayo kwenye shule zetu
na kusimama kwa michezo hiyo na Michezo ya Majeshi (BAMATA).
Michezo
ya Umitashumta/Umisseta ndiyo ilikuwa kiwanda cha kuandaa wachezaji ambapo
wanapofanya vizuri hupata ajira katika taasisi za Serikali (JWTZ, Polisi,
Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa) lakini kwa sasa imekuwa tofauti kwani taasisi
hizo haziajiri kama ilivyo huko nyuma kutokana na kutofanyika Michezo ya
Majeshi (BAMATA) ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa.
Ni
zaidi ya miaka 8 tangu aliporejesha michezo ya Umitashumta/Umisseta kwa nia na
madhumuni ya kupata vipaji vitakavyoendelezwa na kuwa na nafasi nzuri ya
kutuwakilisha Kimataifa.
Imekuwa vigumu kuendeleza vipaji vinavyoonekana katika michezo hiyo
kwani hakuna maandalizi yaliyofanywa kuwaendeleza baada ya michezo hiyo kumalizika. Hata wale
wanaomaliza masomo yao katika ngazi husika hawapati ajira kutokana na taasisi
za Serikali nilizotaja kutokuwa na ajira rasmi kama ilivyo zamani. Mpaka sasa
ni shule chache za binafsi na taasisi
zimekuwa na mpango wa kuwasajili katika
shule zao wanafunzi wazuri wenye vipaji na baadhi yao kutoa elimu bure (Scholarships)
na kuwaendeleza katika baadhi ya michezo:
a.Shule ya Sekondari ya Alliance, Mwanza
(Mpira wa Miguu na Riadha).
b.Shule za Filbert Bayi, Mkuza, Kibaha Mkoa wa Pwani (Riadha na Netiboli)
c.Shule ya Sekondari ya Lord Baden Powel,
Bagamoyo (Mpira wa Miguu kwa Wanaume na
Wanawake, Mpira wa Kikapu, Mpira
wa Wavu na Riadha).
d.Shule ya Sekondari ya Winning Spirit,
Arusha (Riadha)
e.Shule ya Sekondari ya Makongo, Dar Es
Salaam (Mpira wa Miguu, Netiboli Kikapu na Wavu).
Naomba
niishauri Serikali (Wizara ya Elimu na Tamisemi) kuunda Kanda ili kila baada ya
michezo ya Umitashumta na Umisseta wanamichezo wenye vipaji wawekwe katika
shule zilizo katika Kanda zitakazoundwa wakiendelea na masomo hali kadhalika na
kucheza kwa Wizara husika kupeleka wataalamu (coaches) katika Kanda husika.
Kama hilo haliwezekani, basi shule binafsi na taasisi zisaidiwe ili ziweze
kuimarisha zaidi mipango waliyonayo ya kuendeleza michezo
Bila
kuwa na utaratibu na mipango mahsusi, michezo ya Umitashumta na Umisseta, itakuwa kama tamasha tu.
3. UWANJA WA TAIFA
Hakuna
ubishi kwa ushiriki wake katika ujenzi wa uwanja wa Taifa wakati wa uongozi wa
Rais wa awamu ya tatu Mhe. Benjamin William Mkapa akiwa kama Waziri wa Mambo ya
nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mpaka alipochaguliwa kuwa Rais wa awamu
ya nne na kumalizia kazi za ujenzi zilizobaki.
Uwanja
wetu ni mzuri sana, lakini matumizi yake kwa mchezo wa riadha yamekuwa nadra
sana kutokana na gharama kubwa ambayo wakati mwingine Riadha Tanzania inashindwa kuchangia hasa
inapotaka kufanya michezo ya Taifa ambayo hufanyika mara moja kwa mwaka.
Mhe.
Jakaya wakati wa uongozi wake wa miaka 10 kulikuwa na mafanikio ambayo
hayaridhishi kwa nchi kama Tanzania yenye watu zaidi ya Milion 45, lakini
kutokana na hali halisi niliyotaja hapo juu naomba nitaje mafanikio hayo kama
ifuatavyo:
Samson Ramadhani |
1.Samson Ramadhani NYONYI, (Riadha):”Marathon”>Dhahabu: Michezo ya
Jumuiya ya Madola, Melbourne, Australia 2006.
2.Fabian Joseph NAASI, (Riadha): Mita
10000>Shaba: Michezo ya Jumuiya ya Modola, Melbourne, Australia 2006.
Fabian Joseph. |
3.Martin SULLE, (Riadha) Km 21.1>Medali
ya Fedha>Michezo ya Afrika, Algiers, Algeria, 2007.
4.Timu ya Netiboli, (Netiboli)>Medali ya
Fedha>Michezo ya Afrika, Maputo, Msumbiji, 2011.
5.Timu ya Netiboli (Netiboli)>Kushinda
Kombe la Mataifa 6, Singapore, 2012.
6.Timu ya Netiboli (Netiboli>Nafasi ya
Pili, Mashindano ya Africa, Dar Es Salaam, 2012.
7.Timu ya Mpira wa Miguu watoto wa Mitaani
(Street Children World Cup)>Dhahabu, Mashindano Kombe la Dunia, Rio de
Jeneiro, Brazil, 2014.
8.Timu ya Mpira wa Miguu-Vijana chini ya
Miaka 15>Medali ya Fedha> Michezo ya Vijana Afrika, Gaborone, Botswana,
2014.
5. SHUGHULI ZA TOC.
Wakati
wa uongozi wake wa miaka 10 kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Kamati ya Olimpiki Tanzania imeweza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo
kwa vyama vya michezo, baadhi ya hizo shughuli zilikuwa ni kuendesha mafunzo ya
ufundi kwa walimu wa michezo kutoka Vyama/Mashirikisho ya michezo wanachama wa
TOC kwa kuleta Wakufunzi kutoka nje ya nchi hali kadhalika na Mafunzo ya
Utawala na Uongozi wa Michezo kwa viongozi wa Vyama/Mashirikisho ya Mikoa na
Taifa kwa nyakati tofauti.
Kwa
ujumla Walimu 523 (448/75) na viongozi 380 (304/76) waliweza kupata elimu ya
kufundisha wachezaji kwa madaraja tofauti na uongozi na utawala bora.
(Orodha
Nyongeza “A” na “B”imeambatanishwa).
HITIMISHO
Kwa
niaba ya Kamati ya Olimpiki Tanzania na kwa niaba yangu napenda nichukue nafasi
hii kumshukuru Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kutoa posho za
kujikimu, mavazi ya taifa, vifaa vya mazoezi na mashindano timu zetu za Taifa
zilizowahi kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola (Melbourne, Australia 2006,
New Delhi, India 2010 na Glasgow, Scotland 2014) na Olimpiki (Beijing, China
2008, London, Uingereza 2012).
Nitakuwa
mchoyo wa fadhila kama sitamshukuru Mhe. Bernard Camillius Membe, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ushirikiano na WHVUM kuwatafutia
mazoezi ya nje (China, Ethiopia, Uturuki na New Zealand) kwa kutumia mpango wa
Diplomasia ya Michezo (Sports Diplomacy) wanamichezo wetu kabla ya Michezo ya
Jumuiya ya Madola, yaliyofanyika Glasgow, Scotland mwaka jana (2014).
Akiwa
kama mwanamichezo nambari moja hata baada ya kustaafu bado wanamichezo wenzako
tutahitaji ushauri wake katika maendeleo ya michezo katika
nchi
yetu.
Mwisho
kabisa natoa wito kwa wanamichezo wote kujitokeza na kutumia haki yao ya
Kikatiba hapo Jumapili tarehe 25/10/2015 kupiga kura kuchagua mafiga matatu
(Diwani, Mbunge na Rais) kwa kipindi cha miaka 5 (2015-2020) ijayo.
Nawatakia
Wanamichezo wote kila la kheri katika mchakato mzima na tulinde amani tuliyonayo.
Filbert Bayi,
KATIBU
MKUU.
0 Comments